Serikali, imewataka Wafanyakazi wapya 320 wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, ambao walioajiriwa hivi karibuni kwenda kusimamia miradi ya umwagiliaji kikamilifu katika Wilaya watakazopangiwa, ili miradi hiyo ilete tija na kuboresha hali za wakulima nchini.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri Kilimo, Antony Mavunde hivi karibuni na kuongeza kuwa miradi usimamizi mzuri wa miradi hiyo ya umwagiliaji, utaleta matokeo chanya kwenye ukuaji wa Kilimo na kufikia malengo ya kuikuza sekta hiyo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.
Amesema, “bahati nzuri wengi ni vijana chini ya miaka 35 mmeaminiwa na serikali kwenda kuzifanya kazi hizi, itunzeni hii imani kwa maslahi mapana ya Taifa Tanzania, ili mwisho wa siku mkulima wa Tanzania anufaike na ujuzi na maarifa yenu.”
Awali, akitoa maelezo mbele ya hadhara Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa amesema mafunzo hayo kwa waajiriwa wapya yatawajengea uwezo wa kusimamia miradi ya umwagiliaji nchini kote, ili iweze kuleta matokeo chanya katika kilimo.