Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miradi midogo ya umeme inavyobadili maisha vijijini

Mgawo Wa Umeme No Miradi midogo ya umeme inavyobadili maisha vijijini

Thu, 5 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kukamilika kwa mradi wa umeme wa Ijangala unaozalisha kilowati 360 (megawati 0.36) kumesaidia kuinua uchumi kwa wakazi wa vijiji saba katika Wilaya ya Makete, mkoani hapa kwa kuwawezesha wananchi kufungua viwanda vidogo vinavyochochea ukuaji wa uchumi.

Vijiji hivyo ambavyo vinajishughulisha na uzalishaji wa mbao, vina takribani viwanda 100 vya kuchakata mazao hayo ya misitu na idadi hiyo inatazamiwa kuongezeka kwa siku za usoni baada ya kupata umeme wa uhakika.

Mbali na viwanda hivyo, shughuli nyingine za kiuchumi ambazo zinahitaji umeme kwenye vijiji hivyo ni pamoja na kuchomelea, mashine za kusaga, saluni za kike na za kiume ambazo hazikuwepo kutokana na kukosekana kwa nishati hiyo.

Vijiji hivyo vyenye wakazi takribani 4,500 vitakavyonufaika na mradi huo ni Tandala yalipo makao makuu ya mradi huo, Masisiwe, Ikonda, Ihela, Usagatikwa, Ukwama na Ihanga.

Matokeo ya mradi huo yanaonyesha namna gani uwekezaji mdogo unavyoweza kuleta mafanikio na suluhu kwa watu wengi.

Kabla ya kukamilika mradi wa Ijangala mwaka 2021, shughuli hizo zilikuwa zinategemea zaidi nishati ya mafuta, hivyo gharama za uzalishaji na uendeshaji zilikuwa kubwa.

Mmiliki wa kiwanda cha kuranda mbao kilichoko Kijiji cha Masisiwe, Christina Sanga anasema kabla ya kuanzishwa mradi huo walikuwa wanatumia gharama kubwa kufanya shughuli zao, tofauti na ilivyo sasa.

Anasema alikuwa anatumia lita kumi za dizeli zenye thamani ya Sh36,000 (bei ya sasa) kwa siku kwa ajili ya kuendeshea mashine za kuranda mbao zilizokuwa zinaendeshwa na jenereta, tofauti na sasa anapotumia umeme wa Sh2,000 na wakati mwingine pungufu.

Sanga anasema kutokana na gharama za uendeshaji kuwa kubwa, hata bei ya kuchana mbao katika eneo lao ilikuwa ni kubwa tofauti na maeneo mengine yaliyokuwa na umeme.

Anasema kabla ya kuanza kutumia umeme gharama za kuranda ubao wenye urefu wa futi saba ilikuwa ni Sh1,500, lakini kwa sasa wanaranda kwa Sh1,000 na kuchana ubao wa futi 12 ilikuwa ni Sh1,000, sasa ni Sh600.

“Hata bidhaa na samani tulizokuwa tunazalisha kwenye viwanda vyetu zilikuwa zinauzwa kwa gharama kubwa kuliko sehemu zilizokuwa zina umeme na hivyo kufanya uchumi wetu kushuka badala ya kupanda kutokana na wananchi kukimbilia bidhaa zenye gharama ndogo,” anasema Sanga.

Naye Ashura Mtima, mkazi wa Kijiji cha Tandala, Kata ya Tandala anasema kukamilika kwa mradi wa umeme wa Ijangala kumesaidia kurahisisha shughuli za kiuchumi kwenye vijiji vinavyozunguka mradi huo.

Anasema kwa sasa shughuli zote zinazohitajika kufanywa na umeme zinafanyika kijijini hapo, tofauti na awali walipokuwa wanalazimika kusafiri kwenda vijiji jirani kupata huduma hizo.

Mtima anasema kwa sasa wana uhakika wa kupata mwanga wakati wa usiku, tofauti na ilivyokuwa zamani walipokuwa wanatumia vibatari.

Anasema huduma ya kusaga debe moja la mahindi kwenye mashine zinazotumia dizeli ilikuwa ni Sh3,000, lakini baada ya umeme kuingia wanasaga kwa Sh1,000.

Kuongeza nguvu kwenye gridi

Aidha, mradi huo wa Ijangala unaomilikiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Kati (DKK), unatarajiwa kuingizwa kwenye gridi ya Taifa ambapo utapunguza tatizo la kukatika kwa nishati hiyo kwenye Wilaya ya Makete ambayo inategemea umeme wa njia ya Mbeya.

Hilo linathibitishwa na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Nishati Lutheran DKK Investment Limited, Elikana Kitahenga kuwa umeme wa mradi huo unaotokana na mradi huo ambao chanzo chake ni maji ya Mto Ijangala upo kwenye mchakato wa kuingizwa kwenye gridi ya Taifa.

Mkurugenzi huyo anasema mkataba wa kuunganisha umeme huo kwenye gridi ya Taifa kati ya kampuni hiyo na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) umeshasainiwa na kila uniti italipwa Dola za Marekani senti saba (Sh176.05).

Kitahenga anasema mradi huo umegharimu Sh3.9 bilioni na kati ya kiasi hicho, ruzuku ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ni Sh996 milioni, lakini pia waliisaidia kampuni hiyo kupata mkopo kutoka Benki ya Maendeleo TIB.

Anasema katika fedha hizo kanisa ambalo ndilo lenye mradi, limechangia asilimia 10 ya gharama yote ya mradi, huku fedha nyingine zikitoka kwa wahisani wa ndani na nje ya nchi.

"Tumeingia makubaliano na Tanesco kuwa umeme utakaoingizwa kwenye gridi ya Taifa utalipwa Dola za Marekani senti 7 kwa kila uniti, kwa hiyo thamani halisi ya malipo itakuwa inatofautiana kila mwezi kulingana na uniti zitakazoingizwa," anasema Kitahenga.

Kitahenga anasema wazo la kuanzishwa kwa mradi huo lilitokana na changamoto ya ukosefu wa nishati kwa ajili ya kuendeshea shughuli za kila siku.

Anasema shughuli hizo zilikuwa zinahitaji nishati ya umeme na kwa kuwa REA ilikuwa haijawafikia walilazimika kutumia jenereta na hivyo gharama zilikuwa kubwa.

Boss huyo anasema kanisa lilikuwa na vifaa vinavyotumia umeme lakini vilikuwa havifanyi kazi na vilivyokuwa vinafanya kazi vilitumia gharama kubwa ya mafuta kuviendesha, hali iliyosababisha kuja na wazo la kuzalisha umeme kwa njia ya maji.

Anasema kanisa hilo linawahudumia watu wenye mahitaji maalumu pamoja na karakana ya kutengeneza samani ambayo uendeshaji wake kwa njia ya jenereta, ilikuwa gharama kubwa, hali iliyosababisha bidhaa zinazozalishwa kuuzwa kwa bei kubwa kuliko maeneo mengine.

Anasema wakati wazo za kuzalisha umeme linakuja, walikuwa wamepanga kuuzalisha kwa ajili ya mahitaji yao kama taasisi, lakini wakati wa mchakato wakaona kuna uhitaji wa nishati hiyo kwenye vijiji vinavyowazunguka.

“Haikuwa kazi rahisi kama tulivyofikiria, lakini REA walitusaidia kwa hali na mali mpaka hapa tulipofika kwa sababu kama tungetegemea michango ya waumini kukamilisha mradi huu tusingeweza,” anasema Kitahenga.

Mhandisi Miradi REA, Hamisi Mrope anasema wamewezesha mradi huo kukamilika kwa kutoa wataalamu pamoja na ruzuku, ikiwa ni sehemu ya majukumu yao kuhakikisha kuwa umeme unavifikia vijiji vyote Tanzania.

Anasema REA ina jukumu la kuwawezesha wazalishaji wadogo wa umeme ili kufanikisha upatikanaji bora wa nishati ya umeme vijijini kitaalamu na kifedha.

Tanesco Makete

Meneja wa Tanesco Wilaya ya Makete, Henrico Matinde anasema kukamilika kwa mradi wa Ijangala kutarahisisha usambazaji wa umeme kwenye wilaya hiyo ambayo inategemea njia ya umeme kutoka Mbeya.

Matinde anasema kwa sasa usambazaji utakuwa rahisi kwa kuwa chanzo cha umeme zitakuwa hapohapo, hivyo itasaidia kuondoa kukatika kwa umeme kutokana na umbali wa njia ya Mbeya.

Meneja huyo anasema Wilaya ya Makete inakua kwa kasi kutokana na shughuli za kiuchumi zinazofanyika, hivyo umeme wa uhakika utasaidia kurahisisha shughuli hizo.

Anasema shughuli kubwa ya kiuchumi kwenye wilaya hiyo ni kuchana mbao ambayo inahitaji umeme wa uhakika na kuwa njia ya umeme ya Mbeya ilikuwa ikipata hitilafu wilaya yote ya Makete inakosa huduma.

“Mradi huu utasaidia usambazaji wa umeme hasa kwenye vijiji vya Wilaya ya Makete ambapo kuna shughuli nyingi zinazotegemea umeme kama vile kuchomelea, kuranda mbao, saluni za kike na kiume, viwanda vidogo na mashine za kusaga,” anasema Matinde.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live