Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miradi REGROW kuongeza idadi ya Watalii Kusini

Watalii Utaliii Ruaha (600 X 363) Miradi REGROW kuongeza idadi ya Watalii Kusini

Sun, 15 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kukamilika kwa mradi unaotekelezwa na Miradi ya Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania – REGROW, utachochea ongezeko la Watalii wanaoitembelea Hifadhi ya Taifa Nyerere.

Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Benedict Wakulyamba, wakati alipotembelea Hifadhi ya Taifa Nyerere na kukagua miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia REGROW ambapo jumla ya Miradi 22 itakayogharimu zaidi ya shilingi bilioni 141 ikitekelezwa.

Amesema, “Ndugu zangu huu mradi wa Benki ya Dunia wa kuboresha Maliasili zetu unafanya mambo makubwa sana. Kuna changamoto nyingi za uharibifu wa Mazingira yanayosababishwa na shughuli za wananchi na mabadiliko ya tabia ya nchi, sasa mradi huu wa REGROW unaanza kurejesha uhai wa mito yetu katika usimamizi bora wa maji.”

Kwa upande wake Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo ya Biashara, Herman Batiho aliwataka wasimamizi wa miradi inayoendelea kutekelezwa katika Hifadhi ya Taifa Nyerere kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati kwa kufuata viwango vya ubora wa Kimataifa.

“Serikali imejipambanua kupitia Filamu ya (The Royal Tour) juu ya vivutio vyetu, wageni wengi wanakuja na wanataka kuutumia uwanja huu wa ndege, tujitahidi tusiwe kikwazo kwa kukamilisha Uwanja huu ili tuongeze idadi ya Watalii kama ilivyo katika Ilani ya CCM kufikia wageni Milioni tano”, alisema Batiho.

Kwa upande wake Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Nyerere, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi, Ephraim Mwangomo, alisema hifadhi hiyo imejipanga kutekeleza majukumu yake ikiwemo kuendelea kutoa huduma bora kwa watalii na usalama wao pamoja na kushiriki katika kuendeleza jamii zinazozunguka Hifadhi ya Taifa Nyerere.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live