Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miradi 39 yasajiliwa kukuza uchumi Zanzibar

Miradi Pic Miradi 39 yasajiliwa kukuza uchumi Zanzibar

Thu, 8 Dec 2022 Chanzo: Mwananchi

‘Moshi mweupe’ umeanza kutanda katika visiwa vya karafuu baada ya miradi 39 inayohusiana na uchumi wa buluu kusajiliwa na Mamlaka ya Uwekezaji na Ukuzaji Vitega Uchumi (Zipa) katika miaka miwili ya kwanza ya awamu ya nane ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).

Juzi, Mkurugenzi wa Uwezeshaji na Huduma wa Zipa, Shida Makame, akizungumza na waandishi wa habari alisema kati ya miradi hiyo, ya hoteli ni 30 yenye mtaji wa Dola 213.16 milioni za Marekani (Sh490 bilioni), kilimo na uvuvi miradi tisa Dola 18.26 milioni (Sh41 bilioni) na uwekezaji kwenye visiwa 17 Unguja na Pemba ni Dola 414.50 milioni (Sh950 bilioni).

Alisema Mkoa wa Mjini Magharibi unaongoza kwa kupata uwekezaji katika visiwa saba, akivitaja kuwa Kisiwa cha Bawe Dola 30 milioni za Marekani (Sh68 bilioni), Changuu Dola 26 milioni, Kibandiko/Snake Dola 10 milioni na Kwale Dola 68 milioni.

Visiwa vingine katika mkoa huo ni Pamunda ‘A’ Dola 15 milioni za Marekani (Sh34 bilioni), Pamunda ‘B’ Dola 15 milioni na Chapwani Dola 20 milioni.

Mkoa wa Kusini Pemba unafuatia kwa kupata uwekezaji katika visiwa vitano ambavyo ni Misali Dola 83 milioni (Sh190 bilioni), Mtangani Dola 15 milioni (Sh34 bilioni), Kwata Dola 15 milioni (Sh34 bilioni), Kashani Dola 8 milioni (Sh18 bilioni) na Matumbini Dola 15 milioni (Sh34 bilioni).

Shida alisema hadi sasa visiwa vitatu katika Mkoa wa Kaskazini Unguja vimepata uwekezaji ambavyo ni Miwi Dola 25 milioni (Sh57.5 bilioni), Niamembe Dola 7 milioni (Sh16 bilioni) na Mnemba Dola 17 milioni (Sh39 bilioni).

Visiwa vingine ni Pungume Mkoa wa Kusini Unguja Dola 10.5 milioni (Sh24 bilioni) na Njao Kaskazini Pemba ambacho mtaji wa uwekezaji wake ni Dola 15 milioni (Sh34 bilioni).

Halima Wagao, Mkurugenzi Uhamasishaji, Uenezi na Masoko mamlaka hiyo alisema wawekezaji waliojitokeza kuendesha miradi katika visiwa hivyo, wanaendelea na maandalizi, ikiwamo kusafisha maeneo na kukamilisha michoro kabla ya ujenzi kuanza kufanyika mwakani.

Alisema Serikali iko makini kuhakikisha ujenzi katika visiwa hivyo unazingatia uhifadhi wa mazingira ili kuibakisha Zanzibar na uoto asili ambao pia ni miongoni mwa vivutio vya watalii.

Katibu Mtendaji Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Hafsa Hassan Mbamba, pamoja na maendeleo yaliyopatikana, alisema changamoto kadhaa ziliathiri sekta ya utalii katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, ikiwamo Uviko-19.

Chanzo: Mwananchi