KITUO cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimesajili miradi 235 mwaka wa fedha uliopita 2020/21, ikilinganishwa na miradi ya 219 iliyosajiliwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Haya yalisemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji, Geoffrey Mwambe wakati akizungumzia juhudi za Ofisi ya Waziri Mkuu-Uwekezaji na taasisi katika kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kwa kipindi cha Aprili hadi Septemba mwaka huu, mjini Dodoma juzi.
Alisema Tanzania imeendelea kupata mafanikio katika eneo la uwekezaji pamoja na changamoto mbalimbali hasa janga la Covid-19 ambalo limeathiri uchumi wa nchi nyingi duniani na kuwa katika kipindi cha mwaka 2020/21, TIC kilisajili jumla ya miradi 235.
"Katika kipindi cha Machi hadi Agosti, 2021 jumla ya miradi 133 imesajiliwa ikilinganishwa na miradi 105 iliyosajiliwa katika kipindi hicho mwaka 2020 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 27," alisema.
Alisema miradi iliyosajiliwa katika kipindi hicho inatarajiwa kuzalisha ajira 29,709 ikilinganishwa na ajira 8,252 zilizotarajiwa kuzalishwa katika kipindi hicho mwaka 2020.
Alisema miradi hiyo ipo katika sekta ya kilimo, ujenzi majengo ya biashara, nishati, miundombinu ya kiuchumi, taasisi za fedha, rasilimali watu, viwanda, usafirishaji, utalii na huduma.
Mwambe alisema pia kupitia Kituo cha Uwekezaji, serikali imeendelea kufanya maboresho ili kurahisisha uwekezaji nchini pamoja na kuufanikisha uwekezaji katika maeneo ya utoaji wa huduma mahali pamoja, kuboresha mfumo wa kusajili miradi ya uwekezaji, uhamasishaji uwekezaji, kushiriki katika masuala yanayohusu uwekezaji, uwekezaji katika miradi mikubwa ya kimkakati na kusainiwa kwa hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya TIC na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (Zipa).
Aidha, Mwambe alisema pia Ofisi ya Waziri Mkuu, Uwekezaji na taasisi zake imeendelea kutekeleza malengo makuu ya uwekezaji kwa kuweka mwelekeo wa kukuza uwekezaji, maandalizi ya kutunga sheria mpya ya uwekezaji ya mwaka 2021, ushiriki kwenye maandalizi ya vipindi maalumu vya kutangaza fursa za biashara, uwekezaji na utalii.
Alisema pia imeendelea kuboresha mazingira ya biashara kwa kusimamia utekelezaji wa Mpango wa Roadmap wa mwaka 2010 wenye viashiria 11 vya wepesi wa kufanya biashara nchini.
Mwambe alisema Serikali ya Awamu ya Sita pia imeendelea kukuza ushirikiano na sekta binafsi kwa kutangaza fursa mbalimbali za sekta ya utalii zilizopo nchini ili kukuza biashara ya utalii na kuvutia uwekezaji katika sekta hiyo.
Alisema pia imekuwa ikiimarisha majadiliano na utatuzi wa changamoto zinazoikabili sekta binafsi kwa kufanya mikutano ya majadiliano.