Mshauri wa Biashara za Kimataifa na Uwekezaji, Jackson Roselian amesema licha ya mikataba baina ya nchi na nchi (BIT) kuonyesha kuwa inaondoa ubaguzi kati ya mwekezaji mmoja na mwingine, lakini ukweli ina ubaguzi.
Akizungumza katika mjadala wa Twitter space ya Mwananchi leo Agosti 02, 2023 uliohoji umuhimu wa mikataba hiyo, amesema aina ya mikataba hiyo imejielekeza katika kumlinda muwekezaji wa nje na anapewa nafasi kubwa kuliko wa ndani.
“Mikataba inampa upendeleo mwekezaji wa nje, lakini hilo halifanyiki kwa mwekezaji wa ndani,” amesema.
Amesema kwa mara ya tatu mfulilizo kuanzia 2021 hadi 2023 idadi ya BIT zinazovunjwa ni kubwa kuliko nchi zinazoingia makubaliano hayo.
“Hili linafanyika dunia nzima nchi nyingi zimeanza kuona madhara ya mikataba hii ni muhimu kwa Tanzania kuliona hili,” amesema Jackson.
Kwa upande wake, Ofisa Programu, Taasisi ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira (Leat), Clay Mwaifani ameshauri kuboreshwa kwa mifumo ya sheria ili mahakama ziwe huru kufanya kazi zake bila kuingiliwa.
“Tunahitaji huu uwekezaji, lakini uwe unaolenga kulinda maslahi yetu,” amesema.
Amesema iwapo kama Taifa litafanikiwa kudhibiti mitaji na faida isiondoke kwa kiasi kikubwa kama inavyofanyika sasa.
“Tujiulize pia tunapotaka kutoka kwenye hizi BIT je, huu mwelekeo tunaokwenda unatoa majibu ya maswali? Tukisema hatuzihitaji mfumo tunaopendekeza utatupa fursa ya kukata rufaa?” amehoji.