Mikataba 19 imesainiwa wakati wa kufunga Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) itakayohusisha uuzaji mazao na ujenzi wa viwanda.
Mikataba tisa kati ya hiyo, itahusisha ujenzi wa viwanda zaidi ya 500 katika mikoa mitatu nchini na itakagharimu Dola 3 bilioni (ShSh6.9 trilioni), huku vikizalisha ajira 100,000 za moja kwa moja.
Hayo yalielezwa jana jijini Dar es Saalam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Godious Kahyarara wakati akitoa ufafanuzi wa mikataba hiyo.
“Mkataba huo utawezesha ujenzi wa viwanda vikubwa 500 kwa kipindi cha miaka mitatu kwenye kongani ya Kwala mkoani Pwani ambako kutakuwa na viwanda 200, vingine vitakuwa Dodoma na Mwanza,” alisema.
Alisema mkataba huo pia utawezesha ujenzi wa viwanda vya dawa na vifaa tiba, kuunganisha magari, kuchakata bidhaa za mazao, nguo, ngozi na bidhaa.
Mikataba mingine inahusisha uuzaji wa mazao mbalimbali yanayozalishwa nchini, ikiwamo maharagwe ya soya na mahindi. Mikataba hiyo ilisainiwa kati ya kampuni za ndani na zile za nje.
Awali, akifunga maonyesho hayo, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango aliwataka Watanzania kutumia fursa za masoko yanayopatikana nchini kuongeza wigo wa masoko ya bidhaa wanazozalisha.
Dk Mpango alisema ni muda wa wafanyabiashara wa nchini kulitumia vema eneo huru la biashara la Afrika lenye watu zaidi ya bilioni 1.3.
Alisema kutokana na kile alichoeleza kuwa kiwango cha biashara ya Tanzania kwenye masoko ya kikanda ni chini ya asilimia 20, lakini zipo jitihada zinazofanywa na Serikali, ikiwapo kuondoa ushuru wa forodha na kuweka vivutio mbalimbali ili kuongeza uwezo wa kuzalisha bidhaa za nafaka, nyama, samaki, matunda na mbogamboga.
Mpaka sasa Tanzania ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Nchi za Jumuiya ya Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC) na sasa Eneo la soko huru la Afrika (AFcTA).
Dk Mpango alisema ili kufanikisha hilo, wazalishaji wa ndani wanapaswa kuzingatia kanuni za ushindani wa soko kwa kuheshimu mikataba na kuzalisha bidhaa bora zenye viwango huku akiwataka kuongeza uzalishaji.
“Bidhaa kama sukari, mafuta ya kupikia, unga wa ngano na bidhaa za ujenzi; mabati, nondo na saruji, tukidhamiria tunao uwezo wa kujitosheleza kwa mahitaji ya ndani na kuhudumia nje,” alisema.
Aliitaka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara iongeze jitihada za makusudi kubaini vikwazo vya kibiashara visivyo vya kiforodha vinavyokwamisha biashara kati ya Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
“Hasa nchi wanachama wa EAC na SADC zisizoendana na sheria au makubaliano yetu, pia wizara ishirikiane na wafanyabiashara na taasisi ya sekta binafsi kufuatilia utekelezaji wa maagizo ya Rais kwa taasisi za umma kurahisisha mazingira ya ufanyaji biashara hapa nchini,” alisema.
Alizitaka Balozi za Tanzania kuboresha kanzidata ya biashara na fursa za masoko kwa kuhakikisha ni toshelevu na zinapatikana kwa wakati.
“Jana nilitembelea tovuti zenu na kubaini kuwa taarifa za masoko hazijanyumbulishwa kwa ufasaha ili kumwezesha mfanyabiashara mwekezaji kuzitumia,” alisema.
Dk Mpango alitoa shime kwa Wizara za Uwekezaji, Viwanda na Biashara za Tanzania Bara na Zanzibar kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje kuweka nguvu kwenye utafutaji wa masoko kwa bidhaa za Tanzania.
Aliziagiza pia Taasisi za utafiti zifanye kazi ya ziada, ikiwemo kutafuta mbegu za mafuta ya kupikia ambazo zinazalisha mafuta zaidi na kuweka nguvu katika kubuni mashine kwa ajili ya kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa.
Kauli ya Waziri
Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashantu Kijaji alisema wakati nchi ikijiunga AFcTA, walau inacho kitu cha kuanzia huku akiitaja kampuni inayounganisha magari nchini, GFA Trucks.
Alisema tayari Serikali na kampuni hiyo wamekubaliana na wenye viwanda vingine kutumia asilimia 80 ya malighafi zinazotumika zitoke nchi za Afrika na asilimia 50 zitoke Tanzania.
“Tumelibeba hili kwa nguvu zetu zote, tumejifungia sehemu tukifikiri kwa pamoja na wawekezaji hawa kuona tunashiriki vipi na kuingia kama washindani, tutakwenda kulifanyia kazi suala hili,” alisema.