Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mikakati ya Tanzania kuongeza kasi matumizi ya magari ya gesi asilia

Gari Gesi.jpeg Gari iliyofungwa mitambo ya gesi

Thu, 14 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati bei za petroli na dizeli zikipanda Tanzania, Serikali imesema inaangalia uwezekano wa kuwezesha gesi asilia kuuzwa katika vituo vya mafuta nchini ili kuwapatia wamiliki wa vyombo vya moto nishati mbadala yenye gharama nafuu.

Kwa mujibu wa bei mpya za rejereja kwa mwezi Aprili 2022 zilizotangazwa wiki iliyopita na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), mafuta ya dizeli yamepanda kwa zaidi ya Sh250 kwa lita huku petroli ikipanda kwa zaidi ya Sh300 ndani ya kipindi cha mwezi mmoja.

Ewura ilieleza kuwa petroli inayopitia bandari ya Dar es Salaam imepanda hadi kufikia Sh2,861 kwa lita kutoka Sh2,540 iliyokuwa ikitumika Machi 2022 ikiwa ni ongezeko la Sh321.

Bei ya dizeli kuanzia Aprili 6 ilikuwa Sh2,692 kwa lita ikiwa imepanda kwa Sh289 kutoka Sh2,403 ya sasa.

Mkurugenzi wa Petroli wa Ewura, Gerald Maganga aliwaambia wanahabari jijini Dodoma (Aprili 5, 2022) kuwa kupanda kwa bei hizo kumesababishwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na kuongezeka kwa gharama za usafirishaji wa mafuta duniani kulikochagizwa na vita ya Urusi na Ukraine.

Katika kupunguza maumivu ya kupanda kwa bei za mafuta nchini, Msemaji wa Ewura, Titus Kaguo amesema siku zijazo Serikali itaweka msisitizo zaidi katika matumizi ya gesi asilia kama nishati muhimu kwa magari kwa sababu inapatikana kwa wingi nchini.

Amesema mkakati uliopo ni kujenga miundombinu ya kuuzia gesi asilia katika kituo cha mafuta ili kutoa uchaguzi mpana wa matumizi ya nishati za kuendeshea magari, jambo litakalosaidia kuongeza matumizi ya gesi hiyo Tanzania.

“Mipango ya baadaye ni vituo vya mafuta vianze kuuza gesi ili kutoa uchaguzi kwa watu wanaonunua mafuta,” alisema Kaguo Aprili 2, 2022 katika mkutano wa sekta ya mafuta uliowakutanisha wahariri wa vyombo vya habari Tanzania.

Mpaka sasa Tanzania ina vituo vitatu vya kuuzia gesi asilia kwa ajili ya magari vilivyo Tazara na Ubungo jijini Dar es Salaam na kimoja kinachotumiwa na kampuni ya saruji ya Dangote mkoani Mtwara.

Kwa mujibu wa Wizara ya Nishati, uzalishaji wa gesi asilia uliongezeka hadi kufikia futi za ujazo bilioni 56.13 kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai, 2020 hadi mwezi Mei, 2021 ikilinganishwa na futi za ujazo bilioni 53.10 kwa kipindi kama hicho mwaka 2019/20 sawa na ongezeko la asilimia 6.

Hata hivyo, bado mwamko wa kutumia magari yanayoendeshwa na gesi asilia nchini uko chini, jambo linalowakosesha madereva fursa ya kupunguza gharama za nishati na kuchangia katika utunzaji wa mazingira.

Hadi kufikia Aprili 2021, takriban magari 700 yalikuwa yamefungwa mfumo wa matumizi ya gesi asilia ikilinganishwa na magari 400 yaliyofungwa mfumo huo kufikia mwezi Juni, 2020.

Hilo ni sawa na ongezeko la magari 300 au takriban asilimia 75, jambo linalotia moyo katika safari ya kuongeza matumizi ya magari ya gesi asilia nchini.

Sehemu kubwa ya gesi inayozalishwa nchini hutumika kuzalisha umeme unaounganishwa katika gridi ya Taifa na nyingine hutumika katika matumizi ya nyumbani na kuendeshea vyombo vya moto.

Baadhi ya wadau wa sekta ya mafuta akiwemo Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile ameishauri Serikali kubadilisha kanuni zinazosimamia sekta ya nishati na kuweka ulazima wa kila kituo cha mafuta kuwa na miundombinu ya gesi asilia.

Anasema pia kanuni hizo zielekeze magari yote yanayoingia nchini yawe yamefungiwa mifumo na vifaa vinavyoruhusu matumizi ya gesi asilia, jambo litakaloongeza matumizi ya nishati hiyo na kuwapunguzia maumivu watumiaji wa vyombo vya moto.

“Hili suala linaweza kufanyika ndani ya miaka miwili tu maana gesi ipo,” amesema Balile na kubainisha kuwa gesi asilia iliyopo nchini ndiyo inaweza kutatua tatizo la mafuta.

Wadau wengine waliohudhuria mkutano huo uliofanyika jijini Dar es Salaam wamesema Serikali iondoe tozo na kodi kwenye vifaa vinavyotumika kubadilishia mifumo ya magari kutoka mafuta kwenda gesi asilia.

“Serikali inaweza kuweka ruzuku kwenye vifaa vya mfumo wa gesi asili vinavyotumiwa na magari ili kuongeza idadi ya watu wanaotumia nishati hiyo,” amesema Ephraim Bihemo, mwandishi wa habari za uchumi.

Serikali imesema itaendelea kuongeza wigo wa mtandao wa usambazaji gesi asilia na kuifikia mikoa mingine kulingana na upatikanaji wa fedha.

“Serikali imeendelea na utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Matumizi ya Gesi Asilia (NGUMP). Mpango huu ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Nishati ya Mwaka 2015,” ilieleza Wizara ya Nishati katika hotuba ya bajeti kwa mwaka 2021/22.

Katika mpango huo, jumla ya futi za ujazo trilioni 19.7 za gesi asilia zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya matumizi ya soko la ndani katika uzalishaji wa umeme, viwandani, majumbani, taasisi na magari.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live