Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mikakati kuongeza soko la samaki

Uvuvi Tanzaniaaaa Mikakati kuongeza soko la samaki

Wed, 7 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Prof. Riziki Shemdoe amesema wizara yake itaendelea kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), kuhakikisha Sekta ya Uvuvi inakua kwa kuboresha mialo ya samaki wa maji baridi na maji chumvi ili kupata samaki bora zaidi na kuongeza masoko ndani na nje ya nchi.

Prof. Shemdoe amebainisha hayo leo Februari 6, 2024 jijini Dodoma kando ya kikao cha katibu mkuu huyo na wakurugenzi wa halmashauri majiji, manispaa na wilaya zenye shughuli za uvuvi ili kuweka mikakati zaidi ya namna ya kufanya shughuli hiyo kuwa endelevu.

Amesema kutokana na maagizo aliyotoa Rais, Samia Suluhu Hassan hivi karibuni jijini Mwanza wakati wa kukabidhi boti za uvuvi na vizimba ya kuitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kushirikiana na TAMISEMI katika kukuza Sekta ya Uvuvi, tayari maelekezo hayo yameanza kufanyiwa kazi ili kufikia maono ya Rais.

“Leo hii tumekaa kutekeleza kimsingi maelekezo ambayo Rais ameyatoa na tumepata wasaa kuongea na wakurugenzi wa halmashauri na kupanga mipango namna bora ya kuimarisha maeneo ya kupokelea Samaki,” amesema Shemdoe

Amesema baada ya kikao hicho kutakuwa na matokeo chanya yakiwemo ya kupatikana kwa bidhaa bora za samaki ambao watakuwa wanahitajika zaidi kwenye viwanda vya kuchakata minofu ya samaki hivyo kufanikisha zaidi masoko ya ndani na nje ya nchi.

Awali akifungua kikao hicho Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dk Nazael Madalla amesema Sekta ya Uvuvi imekuwa moja ya chanzo muhimu cha mapato kwa halmashauri na taifa kwa ujumla pamoja na kuongeza kipato kwa mtu mmoja mmoja na kuwa kichocheo kikubwa cha uwekezaji.

Wizara ya Mifugo na Uvuvi inaendelea kukutana na wadau mbalimbali kufuatia maono ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kutaka Sekta ya Uvuvi kurasimishwa ili wananchi wanaofanya shughuli zao kupitia sekta hiyo waweze kutambulika rasmi na waweze kunufaika kupitia taasisi mbalimbali za kifedha.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live