Imeelezwa kuwa, Sekta ya Madini ni nguzo muhimu na chachu ya maendeleo ya uchumi wa nchi kupitia rasilimali madini iliyopo nchini.
Hayo yameelezwa leo Oktoba 25, 2023 na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan katika Ufunguzi wa Jukwaa la Madini na Uwekezaji Tanzania 2023 jijini Dar es salaam.
"Kutokana na umuhimu wa Sekta ya Madini katika ukuaji wa uchumi wa nchi yetu, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia uwekezaji zaidi," amesema Dk. Biteko
"Niwahakikishie kuwa, mazingira ya uwekezaji katika Sekta ya Madini yameendelea kuboreshwa na kuwa rafiki zaidi. Nafurahi kusema kuwa, hadi sasa jumla ya Kampuni tisa za Kimataifa za uchimbaji mkubwa wa madini zimeingia ubia na Serikali katika uchimbaji wa madini mbalimbali ikiwemo madini ya nikeli, kinywe, heavy mineral sands (mchanga bahari), Rare Earth Elements, dhahabu na almasi," ameongeza Dk. Biteko
Aidha, Serikali inaendelea kuhakikisha kuwa miundombinu mbalimbali inaboreshwa ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika pamoja na ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema kuwa ili kuhakikisha nchi ya Tanzania inanufaika na rasilimali madini, Wizara itaendelea kuimarisha usimamizi wa shughuli za Sekta ya Madini ili kuhakikisha inawanufaisha wananchi na Serikali inapata mapato stahiki.
Kwa upande mwingine, Mawaziri wa Madini kutoka nchini Malawi, Monica Chang'anamuno na Peter Lokeres kutoka nchini Uganda wamesema kuwa Afrika ina fursa nyingi za Sekta ya Madini zinazovutia wawekezaji kuwekeza.