Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Migodi yenye mikataba na wanaapolo kuorodheshwa            

45b40d0e70a2ebfab95a6cb94c8a8d46 Migodi yenye mikataba na wanaapolo kuorodheshwa     

Sun, 10 Jan 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Zephania Chaula ametoa mwezi mmoja kwa Ofisa Madini Mkazi wa Mirerani, Fabian Mshai na Katibu wa Chama cha Wachimbaji katika Tawi la Mirerani mkoani Manyara(Marema), Rachel Njau, kuorodhesha majina ya wamiliki wa migodi ya tanzanite walioandikishana mikataba ya malipo ya kazi kwa wachimbaji wadogo maarufu, WanaApolo.

Aidha, Chaula ameagiza wamiliki wote wa migodi walioandikishana mikataba ya malipo ya asilimia 10 ya mapato kwa wachimbaji wao na kuwakatia vitambulisho, waandikiwe barua ya kuwapongeza kwa kutekeleza agizo hilo.

Aliyasema hayo wakati akizungumza na wachimbaji wa madini ya tanzanite katika Mji Mdogo wa Mirerani juu ya changamoto mbalimbali zilizowakabili katika mwaka 2020 na zinazotarajia kuwakabili mwaka 2021.

Alisema wanaapolo ni kundi kubwa na lazima maslahi yao yaangaliwe kwa kiasi kikubwa kwani wao ndio nguvu kazi ya kupatikana kwa madini ya tanzanite, hivyo lazima waangaliwe.

Alisema utaratibu huo utaondoa sintofahamu ya baadhi ya wanaapolo kuugua vifua, kisha wamiliki wa migodi kuanza kutupiana jukumu la kuwatibu kama kwamba thamani yao haionekani.

"Mmiliki wa mgodi ambaye hatatekeleza agizo hilo atakuwa amejiweka matatizoni mwenyewe kwani baada ya mwezi mmoja, atafuatilia na kupewa mrejesho wa utekelezaji wake kwenye migodi yote," alisema Chaula.

Aidha, Chaula aliwataka wanaapolo wanaoandikishwa na kupatiwa vitambulisho kutulia katikia migodi husika, badala ya kuhamahama hali inayoshusha uzalishaji na kuwaonesha kuwa hawako makini na hawana msimamo.

Ofisa Madini Mkazi wa Mirerani, Mshai, alisema watatekeleza maagizo yaliyotolewa na mkuu wa wilaya hiyo kwa kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja, wanafuatilia na kuhakiki migodi yote iliyoandikishana mikataba na wachimbaji wake.

"Tutatekeleza maagizo hayo yaliyotolewa na mkuu wa wilaya japokuwa kuna baadhi ya wamiliki walishatekeleza hayo kwa kuandikisha mikataba tofauti kuhusu maslahi ya wanaapolo wanaofanya kazi migodini kwao," alisema Mshai.

Mwenyekiti wa Kamati ya Madini ya Tanzanite Tanzania, Money Yusuf, alisema katika mgodi wake ameandikishana mikataba na baadhi ya wafanyakazi wake kuwalipa asilimia 20 pindi uzalishaji wa madini ukitokea mgodini kwake kulingana na taaluma ya kila mmoja.

"Pamoja na hayo, kuna changamoto kubwa ya baadhi ya wamiliki wa migodi kutakiwa kulipia kodi ya mishahara ya wafanyakazi wao; tunaomba hili liangaliwe kwa umakini zaidi,” alisema Money.

Mmoja wa wachimbaji wa madini hayo, Samwel Rugemaliza alisema bado changamoto ya upatikanaji wa zana za milipuko kwenye migodi ya Tanzanite ni tatizo kwani vibali havitolewi kwa usahihi japokuwa wamelalamikia hilo kwa muda mrefu.

Chanzo: habarileo.co.tz