Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mifuko mbadala kila kona nchini

60960 MIFUKO+PIC

Mon, 3 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Mikoani. Hakuna neno jingine zaidi ya kusema kuwa kilichotokea jana ni hatua ya kwanza ya matumizi ya mifuko mbadala kuonyesha mafanikio sehemu mbalimbali nchini.

Hiyo ni baada ya Serikali kusitisha matumizi, uzalishaji na usambazaji mifuko ya plastiki kuanzia jana kupitia agizo la Aprili 9 mwaka huu lililotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa bungeni jijini Dodoma.

Hata hivyo changamoto zimeibuka katika matumizi ya mifuko mbadala ikiwamo uimara wake, bei, kutopatikana kwa urahisi, changamoto ambazo Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), January Makamba amezitolea majibu.

Makamba jana alizunguka maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam kuangalia mapokeo ya wananchi katika matumizi ya mifuko hiyo.

Alifanya mkutano wa hadhara na wakazi wa Mbagala kwenye viwanja vya Zakhem uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo mkurugenzi mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (Nemc), Dk Samuel Gwamaka.

Kabla ya Mbagala, Waziri Makamba alipita Kariakoo na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara waliomweleza changamoto.

Pia Soma

Awali aliwashuruku Watanzania na wafanyabiashara kwa mwamko mkubwa waliounyesha wa kuachana na matumizi ya mifuko ya plastiki na kutumia mifuko mbadala ambayo ni rafiki kwa mazingira.

Kuhusu upatikanaji mifuko hiyo, Makamba aliwatoa hofu akisema kadri siku zinavyokwenda bidhaa hiyo itapatikana kwa urahisi.

“Wafanyabiashara walishindwa kuwekeza moja kwa moja kwa sababu hawakuwa na uhakika na marufuku rasmi hasa ukizingatia ilishaahirishwa huko nyuma. Lakini baada ya kufanikiwa wengi wameagiza shehena za makontena za mashine ambazo zipo njiani kwa ajili ya utengenezaji wa mifuko mbadala.

“Niwahakikishie baada ya mwezi mmoja mifuko mbadala itachukua nafasi yake na bei itapungua kadri siku zinavyokwenda sababu itakuwa mingi sokoni. Ajira pia zitaongezeka kwa watakaotengeneza na uchumi utapanda,” alisema Makamba.

Kuhusu ubora, Makamba alisema Ofisi ya Makamu wa Rais inashirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), ambao wanaanda miongozo na vigezo kwa wazalishaji na watengenezaji mifuko mbadala.

Makamba pia aliwaeleza watendaji wa Nemc kuwa kesho (leo) hakutakuwa na mapumziko badala yake waende kwenye maduka, magenge na masoko kutoa elimu zaidi kuhusu katazo la mifuko ya plastiki.

Makamba alitumia nafasi hiyo kuwatahadhalisha wanaotaka kutumia mifuko ya plastiki akisema haina nafasi na watabana kila kona.

Naye Dk Gwamaka alisema kuna kampuni tano zimejitokeza kuchukua mifuko ya plastiki itakayokusanywa ili kuzalisha vyombo vya nyumbani zikiwemo ndoo za plastiki.

“Pia kuna viwanda vinne vya saruji vimejitokeza kutaka mifuko hii ili kuitumia kama chanzo cha nishati kwenye uzalishaji wao.

Naye mmoja wajasiriamali wa kuzalisha mifuko mbadala, Jonesia Sebastian amesema kuna mifuko maalumu ya kubebea bidhaa ya nyama na utumbo. “Niwatoe hofu mifuko hii ipo, ni tofauti na ya kuhifadhia nyaraka. Mifuko hii ni migumu ukiweka nyama inakaa zaidi saa mbili bila mfuko kutoboka wala kuloa,” amesema Sebastian huku akipigiwa makofi na waliohudhuria mkutano huo.

Dar es Salaam

Katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam hususan masokoni, kwenye mabucha, soko la Kimataifa la Samaki Feri na madukani, Mwananchi lilishuhudia wananchi na wafanyabiashara wakichangamkia mifuko mbadala.

Mbali na wauza samaki kutumia mifuko mbadala, mama lishe walitumia mifuko ya karatasi kufungia wateja chapati na maandazi.

Muuza samaki Feri, Abdi Othman alisema mifuko mbadala inayotumika sasa inavujisha maji na kusababisha kutoa harufu mbaya.

“Sawa hii ni mifuko inayooza, lakini kwa samaki si rafiki, inavujisha maji, na ili isivuje inabidi tumfungie mteja miwili au mitano na kila mfuko tunanunua Sh500,” alisema.

Katika Soko la Mapinduzi Mwananyamala wafanyabiashara wenye mabucha walilalamikia uhaba wa mifuko hiyo na kusema haifai kufungia nyama.

Shabani Ramadhani muuzaji nyama katika soko hilo alisema mifuko mbadala haifai haipatikani na bei iko juu kitendo kinachosababisha kuwafungia nyama wateja kwenye magazeti.

“Mifuko tuliyoletewa haifai kufungia nyama ukiweka maini au utumbo majimaji yanachuruzika chini lakini mifuko hii ni gharama, inauzwa Sh300 hadi 350,” alieleza Shabani.

Katika soko la Mtambani Kinondoni, Stanslaus Kobero ambaye ni muuza nafaka, alisema wateja walishazoea kwenda sokoni bila mfuko anaponunua vitu unamwekea kwenye mfuko na kuondoka.

“Mifuko mabadala bei iko juu nanunua mifuko 20 kwa shilingi 800 hadi 1,000 anapokuja mteja inabidi kumuuzia Sh200 anapokuwa hana mfuko au hela ya kununua mfuko anaondoka” alisema Kobelo.

Katika masoko ya Tandika na Stereo wanawake wengi walionekana wamebeba vikapu vya kuwekea mahitaji yao.

Mkazi wa Mtoni, Rehema Mbiku alieleza kuwa katazo hilo limewarudisha wanawake nyakati za kubeba vikapu wanapokwenda sokoni.

Arusha wapata soko Uganda

Wafanyabiashara Soko Kuu Arusha wamefanikiwa kupata soko la mifuko ya plastiki na kusafirisha tani 20 nchi jirani ya Uganda ambako marufuku nchini humo bado haijawa na nguvu.

Meneja Soko Kuu Arusha, Magige Makuli alisema katika soko hilo kwa sasa hakuna akiba ya mifuko ya plastiki baada ya wafanyabiashara kupata soko.

“Kulikuwa na akiba ya mifuko lakini wameipeleka Uganda wamepata soko, wenye kiasi kidogo wamesalimisha ofisini zaidi ya kilo 15.” alisema.

Ukiacha changamoto za bei na uimara mifuko hiyo imepokelewa vizuri.

Mbeya nako mambo safi

Jijini Mbeya wananchi wametii agizo kwa kutumia mifuko mbadala. Mwananchi lilishuhudia wananchi kwenye masoko ya Uyole, Soweto na Mwanjelwa wakitumia mifuko mbadala huku wengine wakitumia bahasha za kaki.

Mkazi wa Nsalaga jijini hapa Suzan Mashaka, alisema mifuko iliyoandaliwa na Serikali kama mifuko mbadala si rafiki kwa wananchi ambao ndiyo watumiaji wakubwa wa mifuko ya plastiki.

Mwanza nao walia na bei

Licha ya muitikio lakini wauza samaki na nyama wamelalamikia vifungashio mbadala wakisema havikidhi mahitaji ya wateja wao kwa sababu mifuko hiyo haimudu kubeba bidhaa zenye majimaji.

Hata hivyo, hofu yao iliisha jana baada ya Afisa Mazingira kutoka Baraza la Taifa la Mazingira (Nemc), Abel Sembeka kusema kuwa vifungashio vinavotumika kufungia bidhaa zao vitaendelea kutumika ili mradi viwe na nembo ya TBS.

Kauli hiyo ilimfurahisha mfanyabiashara wa viungo, Salum Abdallah wa Soko Kuu Mwanza aliyesema ruhusa hiyo imewaondolea hofu ya biashara yao kuyumba kwa kukosa vifungashio.

Akizindua rasmi matumizi ya mifuko mbadala na marufuku ya mifuko ya plastiki, mkuu wa mkoa wa Mwanza, John Mongella aliwataka wakazi wa mkoa huo kuvumilia bei zilizopo sasa akiahidi bei zitashuka kadri uzalishaji na uingizaji utakavyoongezeka.

Tanga nako kilio

Mwananchi lilishuhudia jana wakazi wa Jiji la Tanga waliomiminika Soko la Tangamano wakinunua bidhaa zao na kuzihifadhi katika mifuko mbadala huku wakilalamika kuwa inauzwa bei kubwa wakati ile ya plastiki ilikuwa ikitolewa bure.

Mkazi wa Tanga Halima Hassan, alisema mifuko mbadala inauzwa kuanzia Sh300 hadi Sh1,000 wakati wateja wengi wanapokwenda kununua bidhaa wanakuwa na bajeti ya vyakula na si mifuko.

Dodoma ni yaleyale

Omari Abdul mfanyabiashara wa bucha la samaki na nyama katika Mtaa wa Uhindini Dodoma alisema analazimika kuwauzia wateja wake mifuko kwani hata yeye ananunua mifuko hiyo kwa bei ghali.

Alisema bei ya mifuko kumi ambayo ni rafiki kwa mazingira ni Sh3,000 na hivyo kulazimika kuiuza kwa wateja wake kwa Sh300 ingawa kwa upande wake alisema inapatikana kirahisi.

Naye Mariam Sudi alisema alilazimika kuingia gharama ya kununua mfuko wa Sh1,000 baada ya kuambiwa na muuzaji kuwa ajitegemee kwa mfuko.

Moshi walia bei ya mifuko

.Wafanyabiashara wa mifuko mbadala wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro wamelalamikia bei kubwa za mifuko hiyo ikilinganishwa na mifuko ya plastiki iliyokuwa ikitumika kabla ya kupigwa marufuku.

Mwananchi lilipita katika maeneo mbalimbali ya masoko mjini Moshi,na kushuhudia wanunuzi wakiwa wamebeba bidhaa mbalimbali kwenye mifuko mbadala ikiwa ni ishara ya kukubaliana na agizo la Serikali la kupiga marufuku mifuko ya plastiki.

Naye mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira alisema kuwa kwa mkoa huo uzalishaji mifuko mbadala ni mkubwa na inatosha kwa watumiaji wote wa mkoa huo hivyo hatarajii kuona mwananchi yeyote akitumia mifuko ya plastiki.

Imeandikwa na Asna Kaniki, Fortune Francis, Elizabeth Edward (Dar), Mussa Juma (Arusha), Ipyana Samson (Mbeya), Burhan Yakubu (Tanga), Rachel Chibwete (Dodoma), Sada Amir (Mwanza)

Chanzo: mwananchi.co.tz