Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miche 150,000 ya kahawa yagawiwa, kusaidia wakulima

A ZU 4 Y.jfif Miche 150,000 ya kahawa yagawiwa, kusaidia wakulima

Sun, 12 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bodi ya Kahawa Tanzania (TCB) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kahawa nchini (TaCRI) imegawa miche bora ya kahawa zaidi ya 150,000, kwa wakulima katika Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro, lengo likiwa ni kuongeza kasi ya kufufua kilimo cha zao hilo na kuongeza uzalishaji.

Kwa mujibu wa takwimu za TCB, uzalishaji wa kahawa katika Wilaya ya Rombo kwa sasa ni Tani 1,200 na malengo ya ugawaji wa miche hiyo ni kuongeza uzalishaji hadi kufikia zaidi ya tani 4,000 katika Wilaya hiyo, huku malengo ya kitaifa yakiwa ni kuongeza uzalishaji hadi kufikia Tani 300,000 ifikapo mwaka 2025/2026.

Akizungumza leo, wakati wa uzinduzi wa ugawaji wa mche hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa TCB, Kajiru Francis amesema miche hiyo ni ya muda mfupi ambapo mkulima ataweza kuvuna Kahawa baada ya miezi 18.

Kajiru amesema serikali imeweka lengo la uzalishaji wa miche milioni 20 kila mwaka na wamekuwa wakifanya kazi hiyo kwa kushirikiana na TaCRI katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo katika Wilaya ya Rombo vipo vitalu vitatu vya miche bora ya kahawa ambayo itagawanywa bure kwa wakulima.

“Kitalu hiki cha Nanjara kina miche 150,000, na itagawanywa kwa wakulima wa eneo hili na maeneo mengine ya Tarakea bure, lengo likiwa ni kuwapunguzia gharama za uzalishaji na kuongeza uzalishaji wa zao hili, lakini shughuli hii ya ugawaji miche, itaendelea katika maeneo mengine ya Wilaya hii katika kipindi hiki cha mvua, kwani vitalu vipo vitatu vyenye ukubwa huu” amesema Kajiru na kuongeza kuwa

“Miche hii ni ya muda mfupi, wakulima wakipanda baada ya miezi 18 wataanza kuvuna kahawa, lakini ili waweze kufikia lengo hilo lazima waitunze vizuri, na wakulima watambue miche hii ni kama mtu anafuga Ng’ombe wa maziwa, namna unavyomlisha ndivyo unavyopata maziwa mengi, na miche hii namna unavyoitunza ndivyo itakavyowazalishia kahawa nyingi, kuwaongezea kipato na kutimiza malengo ya serikali ya kuondoa umaskini”.

Mtafiti wa usambazaji wa Teknolojia na Mafunzo kutoka TaCRI, Dk Jeremiah Magesa amewataka wakulima kuzingatia kanuni za kilimo na utunzaji wa kahwa ili kuweza kuzalisha kwa tija na kupata bei nzuri.

“Kahawa hizi zinachukua miezi 18, lakini tunasisitiza zaidi wakulima wazingatie kanuni bora za kutunza kahawa, pia maafisa ugani wahakikishe wanawatembelea wakulima na kuwapa ushauri wa kitaalamu ili kuondokana na kilimo cha mazoea na kulima kwa tija” amesema Dk Magesa.

Akitoa elimu ya namna ya kupanda na kutunza kahawa hiyo, Amani Evance ambaye ni mtafiti kutoka TaCRI, amewataka wakulima kufahamu mashamba yao kwa kupima udongo ili kutambua aina na kiasi cha mbolea kinachohitajika na kuondokana na kuweka mbolea kwa mazoea.

“Kipindi hiki cha mvua ndicho kipindi muhimu cha kuotesha kahawa, na katika kuweka mbolea tumekuwa tukishauri mkulima afahamu shamba lake, ili kujua virutubisho vilivyopo kwenye udongo na nini kinahitajika, hiyo inasaidia sana kwani wakulima wengi wamekuwa wakiweka mbolea na kuona haina matokeo kumbe changamoto ni kuweka mbolea ambayo shamba halikuihitaji” amesema Evance

Akizungumza Mbunge wa Rombo ambaye pia ni waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda amesema zao la Kahawa limekuwa linashuka siku hadi siku na sababu ni kupungua kwa maeneo ya kilimo pamoja na watu kupunguza utunzaji wa zao hilo kwa kuona halilipi.

“Niwapongeze TCB na TaCRI kwa kuwezesha kupatikana miche hii bora ya Kahawa, ndugu zangu hii miche inazalisha zaidi kuliko miche tuliyozoea, lakini ili izalishe vizuri ni lazima tuzingatie maelekezo ambayo tunapewa na wataalamu wetu wa Kilimo….naomba Bodi ya Kahawa, ofisa Kilimo wa Wizara na Maofisa ugani tuweke mikakati wa kufanya mafunzo ya utunzaji wa zao hili kwa wakulima”.

“Tunahitaji wataalamu wawafikie wakulima wawape elimu ili waweze kulima kilimo chenye tija na kuyafikia malengo yaliyokusudiwa, kwani kahawa bado ni dhahabu, inalipa lakini tunahitaji kufuata kanuni na taratibu za kilimo na utunzaji”.

Eufemia Masika mmoja wa wakulima wa Kahawa katika Wilaya ya Rombo, amesema ugawaji wa miche hiyo bora utaleta chachu ya kilimo hicho na kuongeza uzalishaji katika Wilaya hiyo na kuwakwamua wananchi kiuchumi.

“Kilimo cha kahawa Rombo kimeshuka sana kwa sababu ya hali ya bei, lakini kwa sasa tumepata elimu na miche hii bora ambayo imefanyiwa utafiti, tunaamini zao hili litarudi kama zamani na watu watarudi kuwekeza kwa wingi kwa sababu litateja tija kwenye jamii”.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live