Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Miamala ya simu na 'eti eti' zake

TOZO Huduma za kifedha kwa njia ya simu

Wed, 18 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mnyukano wa utoaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi, umezidi kupamba moto katika mwaka 2021 na kusababisha baadhi ya kampuni za mawasiliano kupoteza umiliki wa soko na nyingine kujizolea watumiaji wapya.

Mbali na mnyukano huo pia watu 2.86 milioni walianza kutumia huduma za kifedha kupitia simu zao za mkononi mwaka huo.

Kwa mujibu wa ripoti ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) watumiaji wa huduma za kifedha kupitia simu za mkononi waliongezeka kutoka 32.42 milioni waliokuwapo Januari 2021 hadi kufikia milioni 35.28 Desemba 2021.

Kuongezeka kwa watumaji hao kulifanya baadhi ya mitandao kupoteza asilimia za umiliki wa soko lake la huduma za kifedha, huku mitandao mingine ikijivunia ongezeko la wateja.

‘‘Hadi machi 2021 mtandao wa Vodacom ndiyo ulikuwa unaongoza kwa umiliki wa soko la mtandao kwa asilimia 42 lakini hadi machi ilishuka hadi kufika asilimia 40 ya umiliki,’’ ilisema ripoti.

Tigopesa pia ilikuwa ikimiliki soko kwa asilimia 26, Machi mwaka jana lakini umiliki wake ulifikia asilimia 24 Desemba mwaka huu.

Advertisement Wakati mitandao hiyo ikipoteza asilimia za umiliki wa soko, ilikuwa kicheko kwa mitandao mingine ikiwemo Halopesa iliyojipatia ongeze ko la asilimia 2 la watumiaji wa huduma za kifedha.

Umiliki wa Halopesa sokoni ulifikia asilimia 10 Desemba mwaka jana kutoka asilimia nane iliyokuwapo katika robo ya kwanza ya mwaka 2021.

Airtel money wao walipata ongezeko la asilimia moja hadi kufikia umiliki wa asilimia 21 kutoka 20 iliyokuwapo Machi na TTCL walivuna asilimia moja iliyofanya umiliki wa soko la huduma za kifedha kufikia 3.

Wakati mitandao mingine ikipanda mingine ikishuka katika utoaji wa huduma za kifeda kwa upande wa Ezypesa, wao waliendelea kubakiwa na umiliki wa asilimia 2 kati ya robo ya kwanza ya mwaka 2021 hadi robo ya mwisho ya mwaka.

Akizungumzia suala hilo, Dk Olomi Donath ambaye ni mtaalamu wa uchumi na biashara, alisema ongezeko hili limechangiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya wadau kuwa tayari kupokea malipo kupitia simu za mkononi.

Hilo limeenda mbali zaidi hadi kwa wauzaji wa bidhaa ambao wamekuwa wakitumia mitandao katika kutoa huduma zao.

“Inakoelekea itafika wakati watu wataacha kutembea na fedha taslimu, badala yake watakuwa wanafanya malipo kwa njia hii ya kisasa,” alisema Dk Donath. ‘‘Jambo hili lina faida katika uchumi kwani muda ambao mtu alitakiwa kwenda kutafuta fedha benki ili akafanye malipo sehemu fulani anaweza kuutumia muda huo katika shughuli za kiuchumi,’’ aliongeza na kuonya hali hiyo inaweza kupunguza mzunguko wa fedha isiposimamiwa vyema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live