Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mhadhiri aeleza faida ya shina la mkonge

53c358bc780dcf2db8625f7d3370adbb.png Mhadhiri aeleza faida ya shina la mkonge

Wed, 10 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

SEKTA ya mkonge inaweza kuingiza zaidi ya Sh bilioni 10 kwa mwaka kutokana na mabaki ya mkonge ambayo yanaweza kuwa malighafi ya kuzalisha ethanoli kwa ajili ya matumizi mbalimbali hivyo kuwa ni faida kubwa kwa uchumi wa nchi, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya Watanzania.

Mhadhiri Mwandamizi katika Idara ya Sayansi na Teknolojia ya Chakula, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Oscar Kibazohi alisema hayo alipokuwa akitoa mada kuhusu kuongeza thamani kwenye shina la mkonge wakati wa ziara ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa mkoani Tanga hivi karbuni.

Alisema shina la mkonge badala ya kutupwa, kuchomwa moto au kuachwa lioze shambani, linaweza kuongezewa thamani likawa ni malighafi ya kuzalisha bidhaa mbalimbali hasa kemikali kama vile sukari aina ya inulin, uyoga, gesi biologia, chumvi limau, plastiki inayooza, pombe na ethanol.

“Kila hekta moja ina uwezo wa kuzalisha wastani wa tani 23.5 za mashina halisi yaliyoondolewa vikonyo vya majani, hivyo kwa wastani wa hekta 52,000 za mkonge kwa miaka 17 ya maisha ya mkonge, kiwango cha mashina halisi ya mkonge kinachozalishwa kwa mwaka kinafikia tani 72,000.”

"Kiwango hiki kinaweza kuzalisha wastani wa tani 15,000 za sukari aina ya inulin ambayo inaweza kuzalisha tani 5,000 za ethanoli kwa mwaka, iwapo asilimia 75 ya inulin itabadilishwa kuwa ethanol, kwa bei ya jumla ya Sh 1,500 ni sawa na Sh bilioni 10 kwa mwaka," alisema.

Dk Kibazohi alisema zipo changamoto ambazo lazima zifanyiwe kazi na kutolea mfano sukari ya inulin ambayo haibadilishwi na kuwa ethanoli moja kwa moja, bali inabidi ibadilishwe kwanza na kuwa sukari aina ya fructose kama ile inayopatikana kwenye matunda.

"Hii inatakiwa kufanyiwa utafiti, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kipo tayari na kina uwezo wa kufanya utafiti huo," alisema.

Alisema soko la ethanol ni kubwa ndani na nje ya nchi, lakini pia mabaki ya shina la monge baada ya kukamuliwa yanaweza kutengeneza mbao au kuzalisha umeme kama mabaki ya miwa yanavyotumika kuzalisha umeme katika viwanda vya sukari.

Dk Kibazohi alisema zao la mkonge hulimwa nchini katika mikoa ya Pwani, Morogoro na Tanga kwa ajili ya uzalishaji wa nyuzi zinazotumika kutengenezea magunia na kamba.

“Majani ndiyo ambayo yanatumika kuzalisha nyuzi na baada ya miaka 15 hadi 19 huwa yamekatwa yote na hivyo mmea kubakia na shina pamoja na nguzo ya katikati.”

“Ikifika hapo mmea unakuwa hauna thamani tena, shina hukatwa na kuchomwa au kuachwa lioze shambani, shamba kutayarishwa tena na mimea kupandwa upya, hii si sawa,” alisema.

Wiki chache zilizopita Majaliwa alisema wakati umefika wa kurudisha heshima ya mkoa wa Tanga kupitia kilimo cha zao la mkonge na kuwataka wawekezaji na wananchi kuwekeza kwenye kilimo hicho kibiashara.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari), Dk Geofrey Mkamilo alisema kwenye zao hilo taasisi hiyo inasimamia kuongeza uzalishaji kwa kuangalia mbegu bora ambayo inapatikana kituo cha Mlingano.

Alisema ili kutatua changamoto ya uzalishaji wa mkonge, Wizara ya Kilimo kupitia Tari iliandaa mpango wa miaka mitano 2019/20 mpaka 2023/24 wa uendeshaji wa zao la mkonge kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji wa zao hilo katika kuchangia pato la taifa na mkulima.

Chanzo: habarileo.co.tz