Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mohamed Moyo amezima jaribio la wafanyabiashara wa maduka wa mjini Iringa kufunga biashara zao kwa muda usiojulikana kuanzia leo wakilenga kuishinikiza serikali kuwaondoa wamachinga wanaofanya biashara mbele ya maduka yao.
Uamuzi wa wafanyabiashara hao ulianza kutekelezwa mapema leo asubuhi ikiwa imesalia siku moja tu kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuanza ziara yake ya siku tatu, mkoani Iringa.
Rais Samia aliyeko mkoani Njombe kwa sasa, anatarajiwa kuanza ziara hiyo ya kwanza mkoani Iringa kesho Alhamisi toka ashike wadhifa huo.
Hata hivyo machinga wenyewe wameukosoa uamuzi wa wafanyabiashara hao wakisema hauna tija na unalenga kuwakosesha huduma wananchi kwasababu unakwenda kinyume na mipango ya serikali na vikao vyao vya mashauriano vinavyofanyika mara kwa mara.
“Wafanyabiashara hao wanajua tupo tayari kuhamia maeneo rasmi yaliyotengwa lakini wanataka tuhame kabla ujenzi wa miundombinu katika maeneo hayo haujakamilika, hiyo inawezekanaje, wanata twende wapi?” alisema Katibu wa Machinga, Joseph Mwanakijiji.
Mwanakijiji alisema wamekuwepo katika maeneo yasio rasmi kwa maelekezo ya serikali na si kwa bahati mbaya na sasa wanatakiwa kuondoka katika maeneo hayo kwa utaratibu unaopangwa na serikali kwahiyo ni muhimu taratibu za kuwaondoa zikazingatiwa na kuheshimiwa.
Katika kikao chao walichofanya na Mkuu wa Wilaya ya Iringa kupitia Jumuiya ya Wafanyabiashara Iringa, wafanyabiashara hao walisema kuna mambo wamepanga kuyafanya ili serikali kwa upande wake iwathamini kama inavyofanya kwa machinga.
Katibu wa jumuiya hiyo, Cola Mtende aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kufunga biashara kwa muda usiojulikana hadi machinga watakapoondolewa au kutumia nguvu zao wenyewe kuwaondoa bila kujali nini kitatokea.
Mengine ni kususia kulipa kodi na tozo mbalimbali za serikali ukiwemo ushuru wa huduma na kuomba kibali cha kuandamana wakiwa na mabango yenye kero zao ili kufikisha kilio chao kwa Rais.
Akijibu malalamiko hayo, Mkuu wa Wilaya alisema serikali haiwapuuzi wafanyabiashara hao na inathamini na kutambua mchango wao kwa maendeleo ya manispaa, mkoa na Taifa.
Akiwataka wasitishe mpango wao wa kufunga maduka yao na wao kukubali kwa kauli moja, Moyo aliomba hadi Agosti 31, mwaka huu wawe wamekamilisha soko la machinga la Mlandege na kuwahamishia huko.
Naomba mkafungue madukani yenu na muendelee kutoa huduma kwa wananchi. Kufunga maduka ni kuwaadhibu wananchi kwa ujumla wake wanaohitaji huduma kutoka kwenu,” alisema.
Akiahidi kushughulikia changamoto zingine zikiwemo za kodi na tozo, Moyo alisema atafanya vikao vya haraka baina ya wafanyabiashara hao, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na halmashauri ya manispaa ya Iringa ili kuzipatia ufumbuzi.