Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgomo Kariakoo wawaliza Bodaboda

Kariakoo 2 Pic Mgomo Kariakoo wawaliza Bodaboda

Mon, 15 May 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waendesha pikipiki maarufu ' bodaboda' wa Kariakoo wamesema mgomo uliotishwa na wafanyabiashara wa maeneo hayo umewaathiri wakisema shughuli zao zinategemeana na wenye maduka wanawapa kazi ya kusafirisha mizigo yao

Leo Jumatatu Mei 15, 2023, wafanyabiashara wa Kariakaoo wamegoma kufungua maduka yao kwa ajili ya kushinikiza Serikali kuingilia kati utitiri wa kodi wanaotozwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Licha ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala kuwatembea na kuzungumza nao, wafanyabiashara hao wameweka msimamo wa kutofungua maduka hayo hadi watakapoonana na Rais Samia Suluhu Hassan kumweleza kilio chao.

" Siku yetu leo imekuwa mbaya kwa maduka haya kufungwa maana tunategemeana katika shughuli zetu, wao wanatupa mizigo na kuipeleka katika maeneo mbalimbali. Wateja wetu wakuu ni wenye maduka na sio abiria wa kawaida, sasa sijui itakuaje hadi sasa ni saa nne asubuhi bilabila," amesema Gabriel Dominic dereva bodaboda.

Dominic amesema kwa kawaida wenyw maduka huwapa mizigo wanaoipeleka kwa wateja wao maeneo ya Magomeni, Manzese, Sinza,Ubungo, Kinondoni, Mbagala, Tabata na Mwenge, lakini kwa leo hali imekuwa ngumu kwao na hawajui hatima yao.

Naye Mussa Rashid amesema mabosi wao ni wenye maduka wanaowapa kazi zinazosaidia kwa siku kuingiza kipato cha kati ya Sh50, 000 hadi 100,000 kulingana na mwenendo wa oda wanazozipata wafanyabiashara.

"Ninavyozungumza na wewe hadi sasa sijapata hata mteja hata yule wa Sh 2,000 hii si dalili mbaya siku ya leo. Ingekuwa maduka yapo wazi hadi sasa ningekuwa nimeshapata ‘deiwaka’ hata nne na kuingiza kiasi cha kutosha cha fedha.

"Kwa kawaida ukitoa mzigo hapa kupeleka Magomeni gharama yake ni Sh 5,000 au Sinza Sh 7,000 sasa ukienda mara tatu au nne si haba.Sasa leo hali tofauti sijaenda hata safari moja hadi muda huu, hali sio mzuri," amesema Rashid.

Kutokana sintofahamu hiyo, waendesha pikipiki hao wameiomba Serikali kukaa meza moja na wafanyabiashara ili kumaliza mgogoro huo, wakisema umekuwa na athari kwa makundi mbalimbali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live