Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgogoro mgodi wa Tanzanite Mererani mambo magumu

Tanzanite Mnkl.jpeg Mgogoro mgodi wa Tanzanite Mererani mambo magumu

Tue, 28 Mar 2023 Chanzo: mwanachidigital

Mgogoro wa umiliki wa mgodi wa madini ya Tanzanite, eneo la kitalu B, kati ya mchimbaji Patrick Miroshi na mfanyabiashara maarufu jijini Arusha, Japhet Lema umekwama kupata muafaka kutokana na tofauti ya vipimo.

Awali, vipimo vya ofisa madini idara ya vipimo katika machimbo ya Mererani, Elias Azaria akiwa ameongozana na ofisa madini mkazi Mererani, Menard Msengi alipima mgodi huo na kuonyesha upo eneo la Miroshi, lakini Lema alipinga vipimo hivyo na kuomba kupimwa upya.

Upimaji upya ulifanyika jana na kuongozwa na wapimaji ardhi kutoka chuo kikuu cha Dar idara ya vipimo, Sunday Brown na Khaji Komba na vipimo vyao vilionyesha mgodi upo eneo la Lema, lakini Miroshi amepinga.

Miroshi alisema hakubaliani na vipimo hivyo kwani wapimaji wamegharamiwa na Lema, hivyo ana imani na vipimo vilivyofanya na ofisi ya madini Mererani kwa kutumia lesseni yake tangu mwaka 2012.

Ofisa Madini mkazi Mererani, Msengi alisema watatoa uamuzi wa mgogoro baada ya kufanya mapitio ya vipimo vyote na kupitia leseni ya kila mgodi.

“Tuliamua kupata mpimaji huru ili kutatua mgogoro huu, lakini kwa kuwa bado kuna mgogoro tutatoa uamuzi,” alisema.

Msengi awali alikuwa hatambui kama kuna mgogoro baina ya wachimbaji hao, kwani alijua wanachimba kwa ushirikiano katika mgodi huo.

Mgodi unaogombaniwa umekuwa ukimilikiwa na Miroshi tangu mwaka 2012 akiwa na leseni PML 000943NZ na amekuwa akichimba madini na kupeleka kumbukumbu na kodi wizarani.

Hata hivyo, Mchimbaji huyo mwaka 2018 aliingia mkataba na mfanyabiashara Lema kumfadhili kuchimba pamoja katika madini katika mgodi kwa mkataba wa miaka 10. Hata hivyo, mwaka 2020 waliingia katika mgogoro baada ya Lema kutaka kuwa mmoja wa wamiliki. Mgogoro huo ulifikishwa chama cha wachimbaji wadogo wa madini Mkoa wa Manyara (MAREMA) na baadaye Wizara ya Madini, lakini muafaka haukuwahi kupatikana.

Hata hivyo, Februari 13, mwaka huu, maofisa wa madini kutoka wizarani walifika katika mgodi huo na kumweleza Miroshi amekuwa akichimba kwa miaka 11 eneo la mgodi ambalo si lake na wakamuonyesha eneo la pembeni na mgodi wake kuwa ndilo lake na kuwa eneo hilo sasa linamilikiwa na Lema.

Mfanyabiashara Lema akizungumza alikiri alikuwa na mkataba wa miaka 10 kuchimba madini katika mgodi huo wa Miroshi na kueleza amekuja kubaini mgodi huo haukuwa mali ya Miroshi.

Chanzo: mwanachidigital