Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgodi wa dhahabu Singida kuanza uzalishaji mwakani

Kuzama Mgodini Mgodi wa dhahabu Singida kuanza uzalishaji mwakani

Sun, 15 May 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mgodi wa kati wa madini ya dhahabu ulioko Singida, unatarajiwa kuanza rasmi uzalishaji mwanzoni mwa mwaka 2023 baada ya kukamilika kwa ujenzi wa miundombinu ya mgodi huo.

Meneja wa mgodi huo, Jiten Divecha alisema hayo juzi mbele ya Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa wakati alipoutembelea ili kuona maendeleo ya mgodi huo wa Kampuni ya Singida Gold Mine unaomilikiwa na Kampuni ya Shanta Mining Company Limited uliopo Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida.

Divecha alisema mgodi umeendelea kutoa fursa mbalimbali za ajira kwa Watanzania pamoja na kununua bidhaa za Kitanzania. Akizungumza mara baada ya kukagua maeneo ya uchimbaji katika mgodi huo, Dk Kiruswa aliagiza uongozi uhakikishe unamaliza changamoto zote zinazokwamisha kuanza kwa mradi huo ili uchimbaji uanze kwa haraka.

Alisema wananchi wa Ikungi na wakazi wa Singida kwa ujumla wanatarajia kuona mgodi huo unaanza kazi ili waweze kunufaika nao. Dk Kiruswa aliipongeza Kampuni ya Shanta kwa uwekezaji mkubwa wanaoendelea kuufanya katika mgodi huo ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya mgodi, ajira zinazotolewa, afya na miradi mbalimbali ya maendeleo. Vilevile, Dk Kiruswa aliuagiza mgodi huo kuandaa na kutekeleza mpango wa uchangiaji wa kampuni yao kwenye jamii (CSR) kwa mujibu wa sheria.

Alisema wanatakiwa kuhakikisha kama wawekezaji jamii inayowazunguka inanufaika na mradi husika huku akifurahishwa na Sheria ya Local Content inavyotekelezwa na mgodi huo. Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Miraji Mtaturu alimwelezea Dk Kiruswa kuwa wananchi wa Singida wanatamani mradi huo uanze mara moja ili waweze kunufaika na mradi huo.

Alisema mradi utakapoanza utaleta maendeleo kwa jamii inayoizunguka pamoja na kuongeza mapato kwa serikali. Wengine waliohudhuria ziara ya Naibu Waziri wa Madini ni viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Ikungi, viongozi wa vijiji na kata wanaozunguka eneo la mradi na wadau wa sekta ya madini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live