Mgodi wa Dhahabu wa Stamigold uliopo wilayani Biharamulo mkoani Kagera uliokuwa ukijiendesha kwa hasara miaka kadhaa iliyopita sasa umeanza kuokoa Zaidi ya shilingi milioni 700 kila mwezi kuanzia mwezi Aprili mwaka huu.
Mgodi huo ulikuwa ukitumia Zaidi ya shilingi bilioni 1 kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya kuchakata na kuchenjua Dhahabu na sasa baada ya serikali ya awamu ya sita kuweka umeme wa Tanesco mgodini hapo hali inayopelekea mgodi huo kutumia shilingi milioni 300 tu kulipa bili za umeme huku milioni 700 ikitumika kwa matumizi mengine ambayo yalikuwa hayafanyiki.
Akiongea mara baada ya kutembelea mgodi huo, naibu waziri wa Madini Dkt. Stephen Kiluswa ameutaka uongozi wa mgodi huo kutumia pesa wanazookoa kulipia leseni za utafiti ili kuongeza uhai wa mgodi huo.
Dkt. Kiluswa ametumia mwanya huo kuishukuru serikali ya Rais Dkt. Samia kwa kufunga umeme katika mgodi huo na kupelekea mgodi huo kuongeza uzalishaji wenye tija.
Kwa upande wake mbunge wa Jimbo la Biharamulo Mhandisi amesema kuwa uwepo wa mgodi huo Biharamulo jamii inanufaika sana hasa kwa masuala ya kijamii sambmba na kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi wanaozunguka mgodi huo.
Mhandisi Chiwelesa ameushauri uongozi wa mgodi kuendelea kulipia leseni ili mgodi huo uendelee kudumu na kuongeza kuwa uhai wa mgodi huo utatoa mwanga kwa wananchi wa biharamulo hasa wanaoishi karibu na mgodi kuendelea kuwekeza.
Mhandisi Rashid Lulanga ni kaimu Meneja wa mgodi wa Stamigold amesema kuwa kwasasa pesa wanayoipata tayari wameshalipia leseni mbili huku wakiendelea na utafiti ambazo zitaongeza uhai wa mgodi sambamba na kuishukuru serikali kwa huduma ya umeme wa uhakika ambayo hadi sasa imebadirisha mwenendo mzima wa uendeshaji wa mgodi huo.