Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mgodi wa Nyanzaga wahakikishiwa mazingira mazuri

Kijajuuu.jpeg Waziri Biteko akizungumza na Muwekezaji

Thu, 27 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amefanya mazungumzo na ujumbe wa viongozi kutoka mgodi wa Nyanzaga (Nyanzaga Mining Company Limited) uliopo Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza lengo ikiwa ni kupata mrejesho wa maandalizi ya awali kabla ya mgodi huo kuanza uzalishaji.

Dkt. Biteko amefanya mazungumzo hayo akiwa ziarani Kahama mkoani Shinyanga na kutumia fursa hiyo kueleza utayari wa Serikali kuweka mazingira rafiki kwa mgodi huo ikiwemo kufikisha huduma muhimu kama nishati ya umeme, maji na barabara ili kurahisisha shughuli kuanza.

Ujumbe huo kutoka mgodi wa Nyanzaga ukiongozwa na Meneja Mkuu, Damien Valent umemhakikishia Waziri Biteko kuwa maandalizi ya ufunguzi wa mgodi huo yanaendelea vyema ikiwa ni pamoja na kufanya tathmini ya ardhi ili kuwalipa fidia wananchi watakaopisha shughuli za mgodi.

Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Afisa Madini Mkazi Mkoa wa kimadini Kahama Mhandisi Jeremiah Hango, Kamishna Msaidizi Wizara ya Madini Maruvuko Msechu, Kamishna Tume ya Madini Janeth Lekashingo, Afisa Mahusiano mgodi wa Nyanzaga Paul Gongo na Katibu wa mgodi huo Chelestino Malile.

Mgodi wa Nyanzaga ni miongoni mwa migodi minne iliyokabidhiwa leseni za uchimbaji madini mwezi Disemba mwaka jana katika hafla iliyoshuhudiwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambapo unatarajiwa kuendeshwa kwa ubia kupitia kampuni ya pamoja baina ya Serikali na mwekezaji iitwayo Sotta Mining Corporation Limited ambapo Serikali ina hisa za asilimia 16 na mwekezaji asilimia 84.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live