Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfumuko wa bei janga kwa wazalishaji wa chakula

Bei Za Bidhaaa Kupanda.jpeg Mfumuko wa bei janga kwa wazalishaji wa chakula

Thu, 12 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katika hali ya kushangaza kanda zinazoongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini zinatajwa kuwa na kiwango kikubwa cha mfumuko wa bei kuliko zile zenye uzalishaji wa kadiri.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwenendo wa uchumi wa kanda iliyotolewa Oktoba 5, 2023, Kanda ya Kati, Ziwa na Nyanda za Juu Kusini ambazo ziliongoza kwa uzalishaji wa chakula na kuwa na akiba kubwa, mfumuko wake wa bei za bidhaa mwaka 2022/2023 ulikuwa asilimia tano, ukiwa ni wa juu kuliko pengine.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), kapu la kukokotoa mfumo wa bei kwa sehemu kubwa linabebwa na bidhaa za chakula kwa asilimia 28.2 zikifuatia makazi na nishati (maji, umeme, gesi na mafuta) ambayo huchukua asilimia 15.1.

Huduma za usafiri hubeba asilimia 14.1, nguo na viatu asilimia 10.8, gharama za utunzaji nyumba asilimia 7.9, migahawa na malazi (hoteli) asilimia 6.6, habari na mawasiliano asilimia 5.4 huku huduma nyinginezo zikipewa uzito wa chini ya asilimia 5.

Mfumuko huo wa bei kwa mwaka 2022/2023 katika kanda hizo uliongezeka hadi asilimia 5 ikilinganishwa na ule uliokuwapo mwaka 2021/2022. Kwa Kanda ya Kati ulikuwa asilimia 2.3, Dar es Salaam (3.5), Kanda ya Kaskazini (2.7), Kusini Mashariki (3.7) na Nyanda za Juu Kusini asilimia 4.2.

Kanda ya Ziwa pekee ndiyo imeweza kupunguza mfumuko wake wa bei kutoka asilimia 6.7 mwaka 2021/22 hadi asilimia tano na kupungua kwa bei ya bidhaa zisizokuwa za chakula kama nguo, viatu kumetajwa kuwa sababu.

Ikilinganishwa na uzalishaji uliofanyika dhidi ya mahitaji, ripoti hiyo inabainisha kuwa Kanda ya Kati mwaka 2022/2023 ilizalisha tani milioni 3.53 za chakula, huku mahitaji yake katika mwaka 2023/2024 yakiwa tani milioni 3.1.

Kanda ya Ziwa ilizalisha tani milioni 6.14, huku mahitaji yakiwa tani milioni 5.03; Nyanda za Juu Kusini tani milioni 5.57 zilizalishwa, huku mahitaji yake yakiwa tani milioni 2.7.

Katika kipindi husika Kanda ya Dar es Salaam ndiyo iliyokuwa na kiwango kidogo cha uzalishaji wa chakula, ikizalisha tani 10,901 wakati mahitaji yake yakiwa ni tani milioni 1.3, lakini wastani wa mfumuko wake wa bei ulikuwa asilimia 4.

“Ingekuwa ni bei ya chakula peke yake, mfumuko wa bei katika maeneo husika ungeshuka kwa sababu uzalishaji unapoongezeka na vyakula vinaongezeka kulinganisha na mahitaji na hivyo bei yake inashuka, lakini kwa sababu mfumuko unajumuisha na vitu vingine kama mafuta, vinafanya bei kubaki juu,” alisema Oscar Mkude, mtaalamu na mchambuzi wa masuala ya uchumi na biashara.

Mkude anasema katika kuangalia mfumuko wa bei wa Taifa, mambo mawili huangaliwa, ikiwemo bei za mafuta na vyakula na vitu vya kawaida katika uchumi kama ukuaji wake.

“Mafuta ni moja ya vitu kikubwa katika kinachosababisha mfumuko wa bei, kwani bei yake inapopanda inaathiri pia usafirishaji wa bidhaa husika, Dar es Salaam inakuwa na ahueni kwa sababu mafuta mengi yanashuka hapa na bei yake inakuwa chini,” anasema Mkude.

Anasema hiyo ndiyo sababu kubwa inayofanya mfumuko wa bei kubaki juu katika maeneo ambayo yana uzalishaji wa bidhaa za chakula, wakati watu walitarajia ndiyo yangekuwa na mfumuko wa chini.

Hivyo, anasema “mikoa ambayo inaonekana kuwa na asilimia kubwa ya mfumuko wa bei na ina chakula kwa wingi, hali ingekuwa mbaya zaidi ikiwa isingekuwa na chakula,” anaongeza Mkude.

Kwa upande wake Joyna Mgeni, mkazi wa Mpanda anasema changamoto kubwa ni wafanyabiashara kufuata bidhaa hadi mashambani na uuzaji wa chakula nje ya nchi, hali inayoongeza ushindani wa bei katika maeneo ya uzalishaji.

“Mwisho wa siku watu wanauza karibu kila kitu kwa wachuuzi na kusahau soko la ndani la eneo husika, hii inafanya wakazi hao kuendelea kuumia na wanaokwenda kupata ahueni ni wale wasiokuwa hata na mashamba,” anasema Mgeni.

Akizungumzia suala hilo, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Yohana Lawi anasema zipo sababu tofauti zinazoweza kufanya maeneo hayo kuwa na mfumuko mkubwa wa bei licha ya kuwa na uzalishaji mkubwa wa chakula, miongoni mwake ikiwa ni gharama za uzalishaji.

Gharama hizo za uzalishaji zinaangukia sana katika upatikanaji wa pembejeo za kilimo kama mbolea na dawa.

“Pia kuna suala la wafanyabiashara wanaokwenda katika mikoa inayofanya uzalishaji wa mazao ambao wanafanya kuwepo kwa uhitaji mkubwa wa bidhaa na kwa sasa hakuna udhibiti wa kisera, hivyo hii inaweza kuchangia,” anasema Dk Lawi.

Suala la kupanda kwa bei za mafuta nalo lilitajwa kama moja ya sababu huku ikielezwa kuwa ahueni ya mkoa wa Dar es Salaam inatokana na watu kukimbilia kuleta bidhaa zao katika masoko yanayopatikana hapo.

“Lakini ukiangalia asilimia ya mfumuko wa bei za maeneo husika, hata ile ya kitaifa, bado si asilimia kubwa, hii inaonyesha kuwa bado tuko vizuri ukilinganisha na nchi jirani,” anasema Dk Lawi.

Bidhaa viwandani

Eneo jingine linaloangaziwa na ripoti hiyo ni mapato ya viwanda, kikisema licha ya kutoonekana katika uzalishaji wa mazao ya chakula, Mkoa wa Dar es Salaam unakusanya zaidi ya nusu ya mapato yote yatokanayo na uuzaji wa bidhaa za viwandani.

Dar es Salaam iliingiza zaidi ya Sh7.22 trilioni sawa na asilimia 52 ya mapato ya mauzo ya bidhaa za viwandani katika mwaka ulioishia Juni 2022/2023, ikifuatiwa na Kanda ya Kusini Mashariki iliyoingiza zaidi ya Sh2.22 trilioni.

Kanda ya Kati ilikuwa na Sh942.7 bilioni sawa na asilimia 6.9, Kanda ya Ziwa Sh955.7 bilioni huku Nyanda za Juu Kusini ikiingiza Sh739.5 bilioni.

Mauzo hayo ni yale yaliyopatikana katika uuzaji wa bidhaa za vinywaji, unga wa ngano, chuma, sukari, sigara, mbogamboga, sabuni, vifaa vya ujenzi, nguo, magodoro na bidhaa za plastiki.

Kuhusu hilo, Mkude anasema Dar es Salaam inaonekana kuwa na ahueni kwa sababu bidhaa nyingi zinazalishwa hapo na kupelekwa mikoani.

Hata hivyo, anasema kupanda kwa dola kunawagusa watu wa kanda zote, kwa kuwa kunaongeza gharama za uzalishaji, jambo ambalo litafanya watumiaji wa mwisho wa bidhaa ambao wanaishi mikoani kubebeshwa mzigo wa bei.

“Lakini kipindi cha uzalishaji pia huwa kunakuwa na mahitaji makubwa ya bidhaa, ndiyo muda ambao watu wanakuwa na fedha za kununua vitu, wauzaji ni walewale hivyo kunafanya mahitaji kuwa makubwa na kuweka mabadiliko ya bei,” anasema Mkude.

Njia za kukabili mfumuko wa bei

Wakati hali ikiwa hivyo, Mchambuzi wa masuala ya Profesa Samuel Wangwe anasema namna ya kumaliza changamoto ya mfumuko wa bei ni kuongeza uzalishaji wa chakula kwa tija ili kuongeza usambazaji.

“Unaweza kuona sehemu kuna uzalishaji mkubwa wa chakula lakini si kile wanachokula, hivyo mahitaji ya chakula kwao yanaendelea kuwa makubwa, muhimu ni kuongeza tija kwa ujumla wake katika maeneo yote ya uzalishaji ili kuimarisha usambazaji wa chakula nchini,” anasema Profesa Wengwe.

Anaongeza kuwa mbali na kuongeza uzalishaji, ni muhimu kuwa na viwanda vya kuongeza thamani ili bei zisiwe zinashuka na kupanda kulingana na msimu.

Hoja ya Profesa Wangwe inaungwa mkono na Mhadhiri wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Abel Kinyondo anayesema uongezaji thamani mazao ni mwarobaini wa kudhibiti mfumuko wa bei.

Alisema badala ya mtu kuuza mahindi na kusubiri kuuziwa unga uliofungashwa kwa bei ambayo ni mara mbili ya ile aliyouza awali, wakulima wawe watu wanaouza kitu kilichoongezwa thamani.

“Kinacholeta bei kuwa kubwa ni uwezo wake mdogo wa kuongeza thamani, nyie mnatengeneza chakula lakini mnaishia kuuza kile alichokitoa shambani, mwingine ananunua anaenda kuongeza thamani anakuja kukuuzia tena, hili zamani halikuwapo kwa kiasi kikubwa kwa sababu wazee wetu walikula vitu vya asili, tofauti na sasa tunataka vilivyoboreshwa,” anasema Profesa Kinyondo.

Kwenye mafuta ambayo yanatajwa kama sababu ya mfumuko wa bei, Profesa Kinyondo anasema ni vyema Serikali ikajifunza kutumia uhusiano ulioimarika sasa na nchi za Kiarabu ili usaidie kuleta ahueni kipindi kama hiki.

“Tunaposema tuko Dubai, Oman tuwaambie wenzetu kuwa mafuta yanapiga uchumi wetu, tunaomba unafuu kwa sababu sisi ni rafiki zenu, tunapokuwa tunaboresha huu ushirikiano na sisi tuseme tunataka nini,” amesema.

Pia alishauri kuwa ni vyema kuwapo na maghala ya akiba kubwa ya mafuta katika mikoa tofauti ili kuweka ahueni katika maeneo husika.

“Au iwekwe ruzuku kama Kagera bei itaongezeka kwa Sh800 na Dar es Salaam imepanda kwa Sh200 basi Serikali iweke ruzuku ya Sh600 kwa Kagera ili kuweka usawa wa bei,” alisema.

Hata hivyo, alisema matumizi ya nishati mbadala kama gesi asilia katika kuendesha magari, kuzalisha umeme, kuendesha mitambo inaweza kuwa suluhisho la kudumu kuondokana na kilio hicho.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live