Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfumo utoaji risiti TRA unachangia kukwepa kodi

524ef7010d67d8aec2c54ac79956ce89 Mfumo utoaji risiti TRA unachangia kukwepa kodi

Thu, 18 Aug 2022 Chanzo: Habarileo

Wafanyabiashara mbalimbali wa Temeke, Dar es Salaam wameiomba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kuangalia upya mfumo wa utoaji risiti kwa kutumia mashine ya kielektroniki EFDs kwamba unachangia wafanyabiashara wengi kukwepa kulipa kodi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti leo, wafanyabiashara hao wamesema uendeshaji wa mashine hizo ni gharama kubwa kwani kila mwezi wanatakiwa Sh 150,000, kwa ajili ya matengenezo na endapo wakishindwa kutoa fedha hizo kwa wakati, wanafungiwa mfumo na mamlaka hiyo kuwatoza faini.

Katibu wa wafanyabishara wa wilaya hiyo, Prosper Macha amesema asilimia kubwa ya wafanyabishara waliopo hawajui kama wanastahili kutumia mashine hizo kisheria kutokana na mauzo wanayoyapata kwa mwaka.

"Wafanyabishara wanaogopa mashine hizi kutokana na gharama zake, kwa sababu mbali na kulipa kodi na gharama nyingine kwa mwezi anatakiwa kulipa zaidi ya sh milioni tatu, hali hii si kuwakuza bali kuwakandamiza wafanyabiashara," amesema Macha.

Ameeleza endapo TRA itaondoa vikwazo vinavyosababisha wafanyabishara kushindwa kulipa kodi, wataweza kukusanya kodi nyingi.

Mfanyabiashara wa chuma, Mbwana Makame ameishauri mamlaka hiyo kupokea mashine za kielektroniki ambazo wafanyabiashara wananunua na kuzisajili katika mfumo wao, ili kurahisisha utoaji wa huduma.

Amesema mashine za EFD si mbaya, lakini ukiritimba unaofanywa na mawakala wa mashine hizo ndio unaochangia ukwepaji kodi.

Akijibu hoja hizo, Meneja wa TRA Mkoa wa Kodi Temeke, Amina Ndumbogani amesema kuwa mfanyabiashara anayepata mauzo ya kuanzia Sh milioni 11, anatakiwa kutumia mashine hizo na kwamba kutotumia ni kukiuka sheria.

Amesema ili kukwepa adhabu za kutotumia mashine hizo, wanapaswa kuzinunua na kutoa risiti zenye bei halali.

"Lengo la kukutana hapa ni kujitambulisha na kusikiliza maoni ya wadau, changamoto kubwa niliyoiona ni matumizi ya mashine ya EFD. Masuala haya ni ya kisera hivyo tutayafikisha kwa uongozi, ili kuona namna ya kuzitatua na kuongeza ulipaji kodi," amefafanua Ndumbogani.

Chanzo: Habarileo