Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfumo utoaji fedha za TASAF kuboreshwa

5d3523cf77e1270bec1868d19db20dda.jpeg Mfumo utoaji fedha za TASAF kuboreshwa

Mon, 13 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi amesema serikali itafanya maboresho ya mfumo wa utoaji ruzuku kwa wanufaika wa fedha za Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini ulio chini ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf).

Alisema hayo juzi alipokuwa akizungumuza na waratibu wa Tasaf kutoka halmashauri za mkoa wa Geita, ikiwa ni mwendelezo wa tathimini ya maendeleo ya miradi inayoratibiwa na kusimamiwa na mfuko huo.

Alisema hatua hiyo inalenga kuondoa mianya ya hujuma na ufujaji wa fedha za kusaidia kaya masikini unaofanywa na baadhi ya waratibu wa Tasaf na kusababisha wanufaika kutopata stahiki zao kwa usahihi na kwa wakati.

“Tumezungumza na Benki za NMB na CRDB kwa ajili ya kuwa na akaunti maalumu kwa walengwa wa Tasaf ambayo haitakuwa na makato ya aina yoyote, si makato ya ATM (mashine ya kutolea fedha), si makato ya mwisho wa mwezi ya kuendesha akaunti, kwa ujumla haina makato yeyote.”

“Kwa hiyo fedha ile inaenda moja kwa moja kwa mlengwa kwa usalama zaidi. Lakini vilevile tuna mfumo mwingine wa kuingiza fedha kwenye simu ambapo mlengwa atatoa fedha ileile inayotakiwa yeye kupokea na fedha ya makato itakuwa imelipwa na Tasaf wenyewe,” alisema na kuongeza:

“Hiyo ina manufaa makubwa kuweza kulipa kielekroniki, inaondoa hatari ya upotevu wa fedha, lakini kwa wale ambao bado kwa namna moja au nyingine hawana akaunti, hawana namba za simu ambazo ziko kwa majina yao, watapewa hundi,” alisema.

Ndejembi alisema wizara hiyo imeielekeza Tasaf kufanyia mapitio majina ya wanufaika wa ruzuku ya kusaidia kaya masikini ili wote wenye sifa waweze kujumuishwa na tayari mchakato umeanza ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Geita, Harun Elikana alisema katika mpango wa kunusuru kaya masikini awamu ya pili, wameandikisha vijiji 166 na mitaa 38 na kupata jumla ya kaya 47,242 na tayari wamepokea Sh bilioni 16.069 kutekeleza mradi huo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live