Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mfanyabiashara madini alipa faini, akwepa kifungo

20306 Madini+pic TanzaniaWeb

Tue, 2 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar Es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu mfanyabiashara wa madini, Hafidhi Jonggradgorn, kulipa faini ya Sh5 milioni au kwenda jela miaka mitano baada ya kupatikana na hatia ya kumiliki madini bila kuwa na leseni.

Hafidhi maarufu Hafidhi Jong mkazi wa Mikocheni, Dar es Salaam anakabiliwa na mashtaka mawili katika kesi ya uhujumu uchumi namba 37/ 2018, likiwemo la kumiliki madini ya vito mbalimbali vyenye thamani ya dola za kimarekani  105,757.

Hata hivyo, mshtakiwa huyo alilipa faini hiyo na kukwpa kifungo.

Hukumu hiyo imetolewa leo  Oktoba Mosi, 2018 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Wilbard Mashauri baada ya mshtakiwa kukiri mashtaka yanayomkabili.

Pia, mahakama hiyo imeamuru madini hayo yataifishwe na yakabidhiwe Tume  ya Madini.

Awali, Wakili wa Serikali Jacqline Nyantore amedai mahakamani hapo kuwa kesi ilikuja kwa kutajwa na upelelezi wa shauri hilo umekamilika.

“Kesi imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wa shauri hili umekamilika. Mkurugenzi wa Mashtaka ( DPP) amewasilisha hati ya kuruhusu kesi  hii isikilizwe katika Mahakama yako na tuko tayari kumsomea maelezo ya awali( PH)" amedai Nyantore.

Wakili Nyantore amedai katika shtaka la  kwanza la kusaidia kutenda kosa, Hafidhi anadaiwa kati ya Januari  Mosi, 2017 na Juni 3, 2018 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, nchi za Falme za kiarabu na India, akiwa sio mtumishi wa umma kwa  makusudi alifadhili biashara ya mchongo wa jinai kwa lengo la kujipatia faida.

Katika shtaka la  pili la  kumiliki madini bila kuwa na leseni, Nyatore amedai Juni 3, 2018 katika eneo la  Mikocheni A, mtaa wa Chwaku, Hafidhi alikutwa na Vito vya madini mbalimbali aina ya Coloured Gemstones yakiwa na uzito wa kilo 67.76, yenye thamani ya dola za kimarekani, 105,757, bila kuwa na leseni wala uhalali wa kumiliki madini hayo.

Mshtakiwa baada ya kusomewa mashtaka hayo, alikiri mashtaka yake, hali iliyopelekea Hakimu Mashauri kuandaa hukumu.

Chanzo: mwananchi.co.tz