Dunia ina mambo, na mambo ndio haya! Ndicho unachoweza kusema baada ya Mfanyabiashara, Oscar Nondo wa jijini Arusha kujenga hoteli ya kisasa iliyomgharimu Sh. milioni 80 kwa ajili ya kulaza mbwa wake.
Makazi hayo ya mbwa ambayo hayakutegemewa na wengi kwenye Jiji la Arusha ambalo ni kitovu cha utalii nchini, yamejengwa eneo la Kwa Morombo jijini.
Akizugumza na Nipashe jana nyumbani kwake, Nondo alisema ameamua kujenga hoteli hiyo ya kisasa kama makazi ya mbwa wake kwa kuwa watu wengi wanaofuga mbwa, wanajenga vibanda visivyo na hadhi kwa ajili ya kuwalaza wanyama hao, jambo ambalo siyo sahihi.
"Mbwa wanahitaji kulala mahali pazuri na kula vizuri kama tunavyokula sisi binadamu, hivyo nimeamua kuwajengea 'Lodge' hii ili nao walale mahali pazuri," alisema.
Mfanyabiashara huyo alibainisha kuwa mbwa anaowafuga nyumbani kwake Kwa Morombo, anawachukua kutok Poland, ambao ni aina ya Shepherd na wengine waliopo kwa wingi wametoka Afrika Kusini.
"Mbwa wanahitaji mafunzo kama tunavyotunza watoto wetu na kila siku lazima kuamka kumjulia hali ili kama anaumwa unaita daktari mara moja anakuja kumtibu," alisema.
Mfanyabiashara huyo alisema kuwa kwa upande wa chakula anawapa nyama ya kuku mara tatu kwa wiki na nyama ya ng'ombe mara tatu kwa wiki kulingana na aina ya mbwa, akifafanua kuwa baadhi hula nyama mbichi na wengine lazima wachemshiwe.
Alibainisha kuwa kwenye nyumba hiyo aliyowajengea mbwa wake, kuna vyumba 10 vyenye uwezo wa kulaza mbwa wawili.
"Lakini nimeanza kutoa huduma ya kulaza mbwa wengine wa watu wanaosafiri au kubanwa kazini kwa gharama ya Sh. 70,000 kwa wiki na wapo wengi wenye uhitaji huu," alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo ameona ipo haja ya kuongeza Lodge nyingine kwa ajili ya kutoa huduma nzuri kwa mbwa kwa kuwa wengi huteseka wanapoachwa ovyo mtaani tofauti na wanapoachwa hapo kwake kwa kuwa hupatiwa huduma ya kuogeshwa, kula vizuri na kulala mahali pazuri.
Kutokana na utajiri kwenye biashara hiyo, aliwataka vijana wenzake nchini, kubuni miradi ya kuwaingizia kipato kwa kuwa fursa zipo na waache kutegemea serikali pekee, bali waajiri, akisisitiza "serikali haiwezi kuwapa kazi vijana wote".
Mbwa wanaofugwa zaidi nchini kwa ajili ya ulinzi ni aina ya Golden Retriever, Rot Wailers, St Bernard, German shepherd na Caucasian Ovcharka.
Wanaofuga wanyama hao kwa minajili ya ulinzi, huwalea kwa kuzingatia vigezo kadha wa kadha ili waibuke bora katika kulinda. Hata hivyo, aina mbili ya mbwa, German shepherd na Caucasian Ovcharka na Caucasian Shepherd au Caucasian Mountain, ndiyo maarufu katika shughuli za ulinzi.