Manajimenti ya Mamlaka ya Rufaa za Zabuni za Umma (PPAA) imeshiriki mafunzo ya siku tano ya Mfumo mpya wa Ununuzi wa Umma kwa Njia ya Mtandao (NeST).
Mafunzo hayo yanafanyika mkoani Iringa, kufuatia kukamilika kwa Moduli ya Rufaa ya malalamiko ya zabuni.
Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa mafunzo hayo, Kamishna wa Sera ya Ununuzi wa Umma, Dk.Frederick Mwakibinga, amesema serikali inaendelea kutengeneza Mfumo wa NeST kwa kuanzia na moduli chache.
Amesema kufikia sasa, mafanikio makubwa yamezingatiwa kupitia moduli hizo, ikijumuisha kuongezeka kwa uwazi, uwajibikaji, na ushindani wa haki.
“Kwa sasa Serikali inaweza kupata taarifa za moja kwa moja za maendeleo ya zabuni, kama vile zabuni ngapi zimeshughulikiwa, thamani yake, zabuni zilizotolewa hadi sasa, na zipi zinaonekana kuwa na masuala yanayohitaji kuingiliwa au kushughulikiwa, tofauti na mfumo wa zamani”amesema Mwakibinga
Mwakibinga amesema, kukamilika kwa Moduli ya Rufaa kunaongeza ufanisi katika mchakato wa ununuzi na ugavi wa umma, na kurahisisha utoaji haki kwa uwazi.
“Kukamilika kwa moduli ya malalamiko na rufaa ni muhimu kwa sababu michakato yote sasa itafanywa katika mfumo wa kielektroniki. Naipongeza Mamlaka kwa sababu moduli hii itasaidia kuongeza kasi ya kushughulikia malalamiko.
Aidha, amesema kila kitu kinafanyika kwa uwazi ndani ya Mfumo wa NeST na wanaamini malalamiko yatapungua.