Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Meli iliyosheheni watalii yatia nanga Pemba

3825fc6f2ff3d338a268c2d6570980d1.jpeg Meli iliyosheheni watalii yatia nanga Pemba

Wed, 29 Dec 2021 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Meli kubwa ya kitalii ya Le Bellot iliyobeba watalii 69 imetia nanga Pemba.

Watalii hao kutoka nchi mbalimbali za Ulaya waliwasili Pemba juzi na kujionea mandhari nzuri ya kisiwa hicho na kutembelea mashamba ya karafuu na viungo vingine pamoja na magofu ya kale.

Ofisa Mdhamini wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Pemba, Zuhura Mgeni alisema ujio wa watalii hao ni fursa muhimu ya kukifungua kisiwa cha Pemba kuingia katika ramani ya sekta ya utalii duniani.

Alisema hiyo ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya Zanzibar Awamu ya Nane chini ya Rais Dk Hussein Mwinyi kuona Zanzibar inapokea idadi kubwa ya

watalii hadi kufikia 500,000 katika kipindi cha miaka mitano ijayo.

Alisema lengo la Kamisheni ya Utalii kwa upande wa kisiwa cha Pemba ni kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia 150,000 kwa mwaka kutoka watalii 35,000.

‘’Kisiwa cha Pemba kimeanza kufunguka katika sekta ya utalii kufuatia juhudi kubwa za kutangaza sekta hiyo kimataifa, matarajio yetu sasa ni kupokea idadi kubwa ya watalii na kufikia malengo ya watalii 150,000,’’ alisema.

Mkurugenzi wa kampuni ya East Africa Holidays inayoratibu safari ya meli hiyo, Duwe Lazaro amethibitisha ujio wa meli hiyo na kusema kisiwa cha Pemba kina nafasi kubwa ya kutangaza utalii wake duniani kutokana na kuwa

na mazingira ya kuvutia na fukwe mwanana.

‘’Meli hiyo ilianza safari zake katika Kisiwa cha Seycheles kutoka Mauritius na kuelekea Kilwa, Pemba hadi Afrika Kusini ambapo matarajio yetu sasa kisiwa cha Pemba kitafunguka katika sekta ya utalii na uwekezaji zaidi,’’ alisema.

Ofisa Mwandamizi wa Kamisheni ya Utalii Pemba, Hamadi Ameir alisema kazi ya ukarabati wa magofu ya kale ikiwamo ya Mkamandume ipo katika hatua za mwisho kukamilika pamoja na mji wa kale wa Mkumbuu ambayo ni maeneo ya vivutio vya watalii Pemba.

Alisema pia juhudi za kuimarisha msitu wa Ngezi kuwa hifadhi ya taifa unaendelea pamoja na kulinda viumbe vilivyomo hatua ambayo itasaidia kwa kiasi

kikubwa kuimarisha utalii wa Pemba.

‘’Tumejipanga kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa lango kuu la utalii na sasa tupo katika hatua ya mwisho ya kukamilisha baadhi ya vivutio ambavyo vitatembelewa na watalii wakati wanapokuwa nchini ikiwamo magofu ya kale,’’ alisema.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Vitega Uchumi na Uwekezaji (Zipa), Sharif Ali Sharif alisema matarajio ya Serikali ya Awamu ya Nane ni kufungua milango zaidi katika uwekezaji na sekta ya utalii kuelekea uchumi wa buluu.

Alisema visiwa vitatu vilivyopo Pemba vimekodishwa kwa wawekezaji hatua ambayo itafungua milango katika sekta ya utalii kwa watalii wengi kuingia kisiwani humo.

‘’Tumekodisha visiwa vitatu katika kisiwa cha Pemba ikiwamo Misali ambapo matarajio yetu makubwa ni kuona Pemba inafunguka katika sekta ya utalii na ujenzi wa miundombinu ya bandari,” alisema.

Ofisa wa Shirika la Bandari Zanzibar aliyejitambulisha kwa jina la Haji Hamadi alisema Bandari ya Mkoani inahitaji upanuzi mkubwa utakaoruhusu meli kubwa zaidi kutia nanga na kushusha mizigo na watalii.

‘’Tunasubiri utekelezaji wa ahadi ya Rais Dk Hussein Mwinyi ya ujenzi wa Bandari ya Mkoani na nyingine katika kisiwa cha Pemba ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kukifanya kisiwa hiki kuwa lango kuu la uchumi na uwekezaji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati,’’ alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live