Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mchimba madini anayesota miaka 21 akipambana

Madini ,wanamke Shujaa.png Mchimba madini anayesota miaka 21 akipambana

Fri, 8 Mar 2024 Chanzo: mwanachidigital

Rachel Njau aliyerithi mgodi huo kutoka kwa baba yake, ni mama watoto wawili, huku akilea pia watoto wanne aliowaasili, anapambana sasa huu mwaka wa 21 akisaka madini hayo na anajipa moyo ipo siku atakuwa bilionea.

“Najivunia kufanya kazi hii ambayo kwa asilimia kubwa inafanywa na wanaume na ni ngumu. Najivunia miaka 16 kuvumilia kuchimba madini hata kama sijapata kitu bado nachimba, hivyo namshukuru Mungu kwa uthubutu nilionao mpaka sasa.”

Hayo ni maelezo ya Rachel Njau (46), mchimbaji wa madini ya Tanzanite na pia ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wachimbaji Tanzania (Tawoma) na Katibu wa Chama cha Wachimbaji Mkoa wa Manyara (Marema) tawi la Mirerani.

Akizungumza na Mwananchi Digital katika mgodi wake uliopo umbali wa zaidi ya kilomita tatu kutoka ulipo ukuta unaozunguka machimbo ya madini hayo maarufu kama ukuta wa ‘Magufuli’ wilayani Simanjiro Mkoa wa Manyara, Rachel ameeleza safari yake ya uchimbaji wa madini tangu akiwa mtoto mdogo.

Rachel aliyerithi mgodi huo kutoka kwa baba yake ni mama wa watoto wawili, huku akilea pia watoto wanne aliowaasili, anapambana sasa ni mwaka wa 21 akisaka madini hayo na anajipa moyo ipo siku atakuwa bilionea.

Anasema kinachompa moyo ni kuona wenzake wakipata na kuwa kuna wanawake wamenufaika na madini, hivyo anaamini zamu yake itafika.

Wakati leo dunia inaadhimisha Siku ya Wanawake, Rechal anajiona mwenye furaha na matumaini ya kufanikiwa, hivyo anajituma kwa bidii akiamini ipo siku atafanikiwa.

“Najipa moyo kama Bilionea Laizer (Saniniu) ambaye ni mchimbaji mdogo wa Tanzanite anayefanikiwa na sasa anashikilia historia ya kupata Tanzanite kubwa kuliko zote.

“Kesho naweza kuwa Bilionea Rachel kwa sababu baruti anazotumia Laizer ndiyo natumia mimi, vijana anaotumia ndiyo natumia mimi pia,” anajipa moyo Rachel.

Rachel ni miongoni mwa wanawake 30 wanaomiliki migodi ya Tanzanite tangu alipoanza kazi hiyo mwaka 2003. Anasema mwaka jana Stamico waliwapeleka China kuangalia fursa za uwekezaji na pia walikutana na wanawake wachimbaji wa mataifa mengine. Anashukuru na kupongeza uwezeshaji huo unaofanywa na Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Safari ya uchimbaji madini

Katika simulizi yake, Rachel anasema miaka ya nyuma akiwa na umri mdogo, baba yake alikuwa anachimba madini hayo na alikuwa na migodi sita ambayo alikuja kunyang’anywa mitano baadaye na kukamatwa kwa kosa la uhujumu uchumi.

Anasema akiwa mzaliwa wa Kijiji cha Msitu wa Mbogo, kilichokuwa kata ya Mbuguni ambayo kwa sasa ni Kata ya Shambalai wilayani Arumeru, baba yake alikuwa mmoja wa wachimbaji wa madini.

“Kijiji chetu kilikuwa kinalima sana mazao na kila Jumapili ilikuwa ni siku ya soko, kwa hiyo wachimbaji wa Stamico (Shirika la Taifa la Madini) walikuwa wanakuja kufanya biashara ya madini na kununua vyakula.

“Enzi hizo nikiwa mdogo, midoli ya kutengenezwa kwa kitambaa nakumbuka dada yangu mkubwa (Happy), alikuwa ananitengenezea midoli ananiwekea magonga (madini chakavu ya Tanzanite) kwenye macho na vimawemawe vinavyong’aa vilivyokuwa vinabaki.

“Baba yangu alikuwa na migodi zaidi ya sita na kipindi hicho walikuwa hawajarasimishwa, ilikuwa ni uchimbaji wa kivamizi, kampuni ya Stamico ndiyo ilikuwa inasimamia miaka hiyo ya nyuma,” anafafanua.

Rachel anasema baba yake pia alikuwa na baa ambayo biashara ya madini ilikuwa ikifanyika hapo.

“Nakumbuka siku hiyo askari walivyokuja kumbe baba alichukua madini yake akayatupa kwenye mfuko wangu ambao una midoli, walivyokagua walikuta na mfuko na walipouangalia ndani walikuta madini na midoli, baba akasema mwenye midoli yupo mimi sijui hayo madini yameingiaje hapo,” anaeleza.

“Walinifuata kama nyumba ya tatu nilikuwa nacheza rede, nilivyoona wameshika ule mfuko tu nikawafuata walikuwa wamevaa kiraia sikujua kama ni askari,” anasema.

Anaendelea kusimulia kuwa polisi walimkamata na kumpakia kwenye gari lao akiwa na baba na dada yake na kupelekwa kituoni.

Anaeleza kuwa mmoja ya askari hao alimwambia chochote atakachoulizwa kuhusu kilichomo kwenye ule mfuko aseme ni cha kwako na kwa kuwa alikuwa anajua mfuko na midoli yake pamoja na magonga.

“Nilisema ni vyangu kwani nilijua kuna midoli na vipisi vidogo vya magonga ya madini, ila siku wameniita polisi walimwaga vile vitu chini nikashtuka mbona kuna madini ya baba makubwa yako pale ila kwa sababu nilishaambiwa sema ni vya kwako nikasema ni vyangu.

“Kwa hiyo naweza nikasema madini yalikuwa kwenye damu kwa sababu niliingia mahabusu, lakini madini hayakuwa ya kwangu ila leo namiliki mgodi wa madini ya Tanzanite na kati ya migodi sita mmoja nilipewa na baba na migodi mingine mitano iliingia Kitalu C ambayo baba hakupewa kwani hawakuwa na leseni,” anasema.

Anaeleza kuwa baba yake alimwachia mgodi huo ambao uko kitalu B (Opec) na kuwa baada ya kueleza vitu vilivyokuwa kwenye mfuko ni vya kwake, Serikali ilivitaifisha na wakaachiwa.

“Pale mwanamke anapothubutu anaweza kufanya chochote naamini, hata kuendesha magari makubwa watu walikuwa wanajua ni wanaume, kwenye umeme watu walikuwa wanajua ni wanaume, lakini leo wanawake wanapanda juu, ile dhana ya mfumo dume ya zamani,” anasema Rachel.

Anasema kazi ya madini inahitaji uthubutu na kujiamini na kuwa anaamini wanawake wakitumia fursa vizuri wanaweza kunufaisha jamii, huku akitolea mfano baadhi ya wanawake wachimbaji wamejenga zahanati na wengine wamenunua gari la wagonjwa.

Ratiba ya kazi

Anasema ratiba yake ya siku huanza saa 12 asubuhi kwa kuingi geti la ukuta wa Magufuli likifunguliwa na kuisha saa mbili usiku.

“Naingia geti likifunguliwa saa 12 asubuhi, ikifika saa moja kasoro naondoka narudi nyumbani kujiandaa, naingia ofisini (ofisi ya chama cha wachimba madini), kisha mchana narudi mgodini, natoka hapa mgodini vijana nikishaongea nao, nakwenda kulea familia. Ikifika saa 10 alasiri nakwenda shambani msitu wa mbogo hadi saa 2 usiku narudi nyumbani,” anasema.

Anasema ratiba hiyo huwa ni ya siku sita, isipokuwa Jumapili ambayo huitumia kushinda kanisani.

Changamoto

Kuhusu changamoto, anasema kama mchimbaji mwanamke ni kutokwenda mpaka mgodini chini (manta), hivyo kunaweza kuwa na uwezekano mkubwa wa kudanganywa.

Changamoto nyingine ni ukosefu wa mtaji wa kutosha, kwani uchimbaji unatumia gharama kubwa na wenye uwezo wa kununua vifaa huweza kuchimba vizuri na kupata madini.

Akieleza jinsi anavyokabiliana na changamoto hizo, Rachel anasema, “kumbuka mimi siendi manta mpaka kule chini, hamna mwanamke anayezama hiyo ni changamoto, lakini ninavyokaa na wale vijana ni kama watoto niliowazaa, shida yoyote waliyonayo iwe ya kifamilia, mgodini lazima nihakikishe nimeitataua naishi nao vizuri.

“Kila iitwapo leo, tunazimudu changamoto kwa sababu tunaipenda hii kazi, ukiipenda kazi utajua jinsi gani ya kutatua.”

Kuhusu gharama za uchimbaji, anasema inategemea na unavyochimba na kuwa kuchimba inategemea unatumia matundu mangapi, ukishajua utajua unatumia kiasi gani na vitu vingine.

“Kwa hiyo kila mtu anayechimba ana matumizi yake, mfano mimi nikiwa na milioni moja naweza nikafanya kazi wiki nzima, nitakuwa na boksi la mafuta laki mbili, kamba ambayo ni milioni moja ukinunua jumla, nikiwa na milioni naweza kufanya kazi kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa hapo nimejibana,” anasema.

“Mimi naweza kuzamisha viroba vya kuwekea udongo na viroba ni Sh2,000 mwingine anazamisha viroba 10,000 kwa hiyo kwenye uchimbaji kuna utofauti na wote tunatumia gharama.

“Uchimbaji una gharama kubwa sana kuliko mtu anavyofikiri, a mtu anaweza akakaa miaka 25 hajapata, lakini akipata anapata kwelikweli, anasahau ile miaka 25 tofauti na kwenye dhahabu kila siku watu wanapata kidogo kidogo, sisi hatupati kabisa,” anafafanua.

Mchimbaji huyo anasema hadi sasa ana vijana 30 wanaosaidia shughuli za uchimbaji, ila kwa sasa wapo wachimbaji 20 ambao anasubiri kutoa udongo mgodini na kuwa licha ya kwamba amechimba kwa miaka 16, bado hajapata ila anajivunia uthubutu alionao.

Chanzo: mwanachidigital