Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mchengerwa azipa neno TTB, Tanapa

Mchengerwa Mbarali Pic Mchengerwa azipa neno TTB, Tanapa

Tue, 22 Aug 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Mohamed Mchengerwa amezitaka Bodi za Utalii (TTB) na Bodi ya Udhamini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kuondoa utendaji wa mazoea katika sekta hizo na kutumia uzoefu kuhakikisha matarajio ya sekta hiyo yanafanikiwa.

Miongoni mwa matarajio hayo ni pamoja na kuhakikisha Tanzania inakuwa namba moja Afrika na katika sekta ya utalii.

Mchengerwa ametoa kauli hiyo akiwa jijini Arusha katika uzinduzi wa bodi mpya ya TTB na TANAPA. Waziri Mchengerwa alisikitishwa kuona taifa likiwa na vivutio vingi vya utalii ila inaingiza watalii wachache, alitaka kuwepo jitihada za pamoja kuongeza watalii.

Alisema TANAPA na TTB ni sekta muhimu na malengo ya Wizara ya Maliasili na Utalii na serikali katika malengo yake hadi kufikia mwaka 2025 inataka kuingiza watalii zaidi ya milioni tano na mapato ya zaidi ya Sh bilioni 6 kwa hiyo mipango madhubuti ya kutangaza vivutio vya utalii inahitajika.

Mchengerwa alisema bila kutangaza utalii ndani na nje ya nchi malengo ya serikali hayatofanikiwa hivyo ni wajibu wa bodi hizo kuhakikisha ina kaza buti usiku na mchana kuhakikisha malengo yake yanafikiwa.

‘’Kazi kubwa ya wenyeviti wa bodi ni kuhakikisha malengo ya wizara na serikali yanafanikiwa kwa maslahi ya nchi na kwenda kusimamia mashirika hayo kufanya kazi na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.’’alisema Mchengerwa.

Mbali ya hilo alizitaka bodi hizo kukaa na menejimenti ili kufanya mapitio ya sheria zinazoonyesha kukizana na malengo ya maboresho ya sekta ya utalii ili kuleta mapinduzi makubwa.

Waziri Mchengerwa amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa maono yake ya kuifungua na kuitangaza Tanzania na vivutio vyake kupitia filamu ya The Royal Tour na kuwataka wenyeviti wa bodi kubuni mbinu na mikakati ya kuvutia watalii zaidi hapa nchini.

“Rais aliamua kutufungulia njia kwa kuanzisha Programu maalum ijulikanayo kwa jina la Tanzania: ‘The Royal Tour’ inayolenga kutangaza vivutio vya utalii na fursa za uwekezaji.

Hivyo, tunao wajibu wa kuhakikisha kuwa programu hiyo inakuwa endelevu sambamba na kuanzisha mikakati mbalimbali itakayochochea ongezeko la watalii nchini pamoja na mapato yatokanayo na sekta ya utalii.” alifafanua Mchengerwa.

Kwa upande wa Bodi ya TANAPA ametoa wito kuendelea kusimamia mfumo wa kijeshi ili kufikia malengo ya kuanzishwa kwa Jeshi la Uhifadhi hususani katika eneo la uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori na misitu katika maeneo ya hifadhi zote.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live