Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mchango wa madini pato la taifa wafikia asilimia 7.9

6b4b8ed579ba766cfd10a030ca8f6751.PNG Mchango wa madini pato la taifa wafikia asilimia 7.9

Fri, 11 Mar 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Madini, Dk Doto Biteko alisema chini ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita, mchango wa sekta ya madini katika pato la taifa umeongezeka hadi kufi kia asilimia 7.9 huku madini yenye thamani ya Sh trilioni 8.3 yakiuzwa.

Dk Biteko alisema hayo wakati wa kuzungumzia mafanikio ya mwaka mmoja ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya madini.

Alisema mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa umekuwa ukiongezeka kutoka robo moja ya mwaka hadi nyingine na katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka 2021 wastani wa mchango umekua hadi kufikia asilimia 7.3 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na wastani wa asilimia 6.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

Dk Biteko alisema katika robo ya tatu ya Julai hadi Septemba mwaka 2021, mchango wa sekta ya madini umeongezeka hadi kufikia asilimia 7.9 kutoka asilimia 7.3 ya Pato la Taifa katika kipindi kama hicho mwaka 2020.

“Matokeo haya yanaakisi dhamira ya Serikali kuhakikisha sekta hii inaimarika na kuweza kuchangia Pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025,” alisema.

Kuhusu mauzo, Dk Biteko alisema Serikali ya Awamu ya Sita imeweka historia kwa kushuhudia mauzo ya moja kwa moja yenye thamani ya Sh trilioni 8.3 kutokana na mauzo ya madini ya aina mbalimbali.

“Mauzo hayo yanatokana na madini ya dhahabu, madini ya fedha, madini ya shaba, makaa ya mawe, madini ya kinywe, madini ya vito na madini ya ujenzi na viwandani,” alisema.

Dk Biteko alisema kutokana na biashara ya madini, Wizara imekusanya Sh bilioni 597.53 kama maduhuli ya serikali yaliyokusanywa kupitia wizara kupitia mirabaha ya asilimia 6 na asilimia moja ya ukaguzi.

“Lakini pia sekta ya madini imekuwa na mchango mwingine kama kodi na tozo mbalimbali, mfano kwa kampuni tatu kubwa za madini zimechangia dola za Marekani milioni 652 ambazo ni sawa na shilingi trilioni 1.5 ikiwa ni kodi na tozo nyingine.”

Aidha, Dk Biteko alisema kwa sasa Wizara imeongeza usimamizi kwenye madini ya ujenzi na viwandani ambapo tayari mifumo ya kielektroniki imeanza kutumika katika usimamizi wa mapato ya Serikali yatokanayo na madini.

“Katika juhudi za kusimamia upatikanaji wa mapato kutokana na madini ya ujenzi na viwandani, Wizara ya Madini imeanza ushirikiano na Wizara ya Tamisemi ili kuwafikia wananchi wanaotumia madini hayo na waweze kuchangia fedha zitokanazo na shughuli za uchimbaji madini hayo kwa mujibu wa Sheria ya Madini,” alisema Dk Biteko.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live