MTAKWIMU Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa amesema takwimu za uchumi zinaonesha mchango wa shughuli za kilimo katika Pato la Taifa umeongezeka hadi asilimia 26.9 mwaka jana ikilinganishwa na asilimia 26.6 mwaka 2019.
Alisema hayo jijini Dodoma jana wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya mwaka wa kilimo 2019/2020.
Dk Chuwa amesema sensa hiyo ni ya tano, ambazo nyingine zilifanyika misimu ya 1971/72, 1993/94 na 1994/95, 2002/03 na ya nne ni ya 2007/08 na kwamba kazi hiyo imekuwa ikifanywa kila baada ya miaka 10.
Alisema kiwango cha ukuaji wa shughuli za kiuchumi za sekta ya kilimo ambazo zinajumuisha mazao, mifugo, misitu na uvuvi zilikua kwa asilimia 4.9 mwaka jana ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.4 mwaka 2019.
Mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri alisema takwimu hizo zitasaidia mipango ya wakulima nchini kuanzia wakati wa kuandaa mashamba, upatikanaji wa mbegu bora kwa wakati, wakati wa mavuno na kuunganisha masoko ya wakulima.
Waziri wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda alisema serikali inatekeleza kwa vitendo Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III: 2021/2022-2025/2026) na Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kwa lengo la kujenga uchumi shindani na viwanda.
Profesa Mkenda alisema utekelezaji wa sera yoyote unahitaji ushahidi wa kisayansi na kwamba takwimu zinazokidhi viwango vinavyokubalika ni msingi muhimu kwa serikali kujipima katika dhana nzima ya kujenga uchumi shindani.
“Mazao ya kilimo yanayozalishwa nchini yanakidhi mahitaji ya chakula cha watu takribani milioni 60 nchini kwa asilimia 100 na uzalishaji huo unatoa ziada kwa ajili ya kuuza nje,” alisema Profesa Mkenda.
Alisema shughuli za kilimo ambazo zinajumuisha mazao, mifugo, misitu na uvuvi zimeendelea kutoa mchango katika kukuza uchumi wa nchi katika mpango wa tatu wa maendeleo wa kujenga uchumi shindani wa viwanda.