Naibu Waziri wa Madini, Stephen Kiruswa amesema mchakato wa mabadiliko ya sheria na kanuni kuhusu biashara ya Tanzanite unaendelea.
Amesema wizara imeshapeleka mapendekezo ya maboresho ya kanuni ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambayo imeahidi kuyatoa Februari 28 mwaka huu.
Naibu Waziri Kiruswa amesema hayo jana Januari 23, 2024 katika mkutano wa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda uliofanyika jijini Arusha.
Awali, katika mkutano huo, mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo aliomba Serikali kuondoa zuio la kuuza madini hayo nje ya Mirerani.
Gambo amesema tayari mazungumzo yamefanyika katika ngazi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wizara ya Madini lakini bado uamuzi haujatolewa.
Kwa muda mrefu wafanyabiashara wa Tanzanite wamekuwa wakitaka kuruhusiwa kufanya biashara ya madini hayo nje ya Mirerani.
Julai 7, 2021 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitoa maelekezo ya Serikali kupiga marufuku biashara ya madini ghafi ya Tanzanite kufanyika nje ya Mirerani.
Hatua hiyo ililenga kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo na kukuza soko la madini la Mirerani.
Uamuzi huo pia ulitokana na maombi ya mbunge wa Simanjiro, Christopher ole Sendeka ya kuzuia biashara ya madini ghafi kufanyika nje ya Mirereni ili kusaidia uchumi wa eneo hilo, pia kuhakikisha wananchi wilayani Simanjiro wananufaika na madini hayo ambayo hupatikana katika wilaya hiyo pekee duniani.
Hata hivyo, wafanyabiashara wa madini hayo na wanasiasa, akiwamo mbunge Gambo na aliyekuwa mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema wamekuwa wakiiomba Serikali ibadili uamuzi huo ili Watanzania wote wanufaike na madini hayo kuuzwa katika masoko ya ndani ya nchi.