Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge, waziri wavutana malipo ya korosho

35037 Pic+korosho Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga

Mon, 7 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mbunge wa Ndanda (Chadema) mkoani Mtwara, Cecil Mwambe amejikuta katika mvutano na Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga baada ya kueleza kile alichodai kuwa ni changamoto zinazowakabili wakulima wa korosho katika mikoa ya Kusini.

Mwambe alisema jana kuwa kuna changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika mchakato wa malipo ya zao hilo unaoendelea kwenye mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani na Ruvuma.

Hata hivyo, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema hayo ni maoni ya mbunge huyo huku, akisisitiza kuwa hayana msingi wowote kwa kuwa Serikali inafanya kazi kubwa ya kuwalipa wakulima wote wa korosho.

Awali, Mwambe katika taarifa yake jana alisema baada ya kufanya uchunguzi binafsi wa kile kinachoendelea kuhusiana na malipo ya korosho, amebaini kuwa hakiakisi kile kinachosemwa na viongozi wa Serikali.

Alisema ni wakati mwafaka kwa Rais John Magufuli kufanya ziara katika mikoa ya Kusini ili akazungumze na wananchi na wakulima wa korosho kupata undani wa kipi kinachoendelea.

“Sasa hivi ukizungumzia suala la korosho unaonekana kama unawatetea walanguzi. Tunamuomba Rais Magufuli aje awasikilize wakulima yeye mwenyewe. Kingine ni vyema vikao vya wadau wa korosho vikaendeshwa kwa uwazi ili kuwasaidia wakulima hawa,” alisema.

Mbunge huyo alidai kuwa wakulima wanaolipwa kwa kusuasua hivi sasa ni wale wenye kilo chache za korosho, lakini wenye tani 1.5 hawalipwi kwa kisingizio cha uhakiki, tofauti na taarifa anazopatiwa Rais Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutoka kwa watendaji waliowatuma kufanya na kusimamia kazi hiyo.

Pia, alidai kuna viashiria vya rushwa wakati wa mchakato wa uhakiki kutoka kwa wahakiki na wakulima ambao wamegawanywa katika makundi, jambo linalowafanya wawe wanyonge.

Mbunge huyo alidai taarifa za malipo zimekuwa siri, jambo linalosababisha baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi kutojua kinachoendelea katika mchakato huo hasa kwa wakulima waliokusanya korosho maghalani.

Kwa mujibu wa Mwambe, changamoto hizo zinaweza kuleta athari pia kwa halmashauri kushindwa kujiendesha kwa sababu zinategemea kwa kiasi kikubwa mapato yatokanayo na mazao ya biashara ikiwamo korosho.

“Itasababisha pia kuharibika kwa korosho zilizoko kwenye maghala kwa kunyeshewa na mvua, hasa zile zilizoko mikononi mwa wakulima,” alisema.

Alisema kama hali hiyo haitadhibitiwa hivi sasa, kuna hatari kwa wakulima kudhalilishwa kwa kushindwa kumudu gharama za maisha na kushindwa kuwapeleka watoto wao shule, jambo litakalosababisha kiwango cha elimu kushuka katika mikoa hiyo.

“Lakini pia wakulima hawa hawa watashindwa kuandaa mashamba yao kwa ajili ya msimu ujao,” alisema mbunge huyo.

Ufafanuzi wa Waziri Hasunga

Akijibu madai ya Mwambe, Waziri Hasunga alisema Serikali inawalipa wakulima kwa jinsi utaratibu ulivyo.

“Serikali inamlipa yule mkulima aliyehakikiwa na kazi hii tunaifanya kwa ufanisi mkubwa. Anaposema kasi ya kulipa imekuwa ndogo nadhani Mwambe anazungumzia mambo ya zamani,” alisema Hasunga.

“Sasa hivi kasi imekuwa kubwa ya kulipa wakulima ndiyo maana kila baada ya muda fulani natoa takwimu kuhusu mchakato huu.”

Alisema, “Kama yeye (Mwambe) na wakulima wengine wanaona kasi ni ndogo, waende benki wakajiridhishe.”

Wabunge mikoa ya Kusini

Mmoja wa wabunge wa mikoa ya Kusini ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini alisema kama vyombo vya habari vinataka kuwasaidia wakulima hao ni vyema vikaenda kuzungumza nao wenyewe na viongozi wa vyama vya ushirika badala ya kufanyia kazi kauli za wanasiasa.

Hata hivyo, akizungumzia madai ya uwapo wa viashiria vya rushwa katika malipo, Mbunge wa Newala Vijijini (CCM), Ajali Akibar alisema hana uhakika kama vipo kama inavyodaiwa na Mwambe.

“Ninachojua bado wananchi wengi hawajalipwa na waliolipwa ni wale wenye kilo ndogo za korosho. Wenye kilo nyingi bado hawajapata fedha zao, ninachowaambia wakulima wawe watulivu na waitii Serikali, nikipata nafasi katika kikao kijacho cha Bunge nitalizungumzia hili,” alisema alisema Akibar.

Mwenyekiti wa wabunge wa Mkoa wa Lindi, Seleman Bungara alisema kilichoelezwa na Mwambe ni sahihi na hali hiyo inaonyesha namna tatizo lilivyo kubwa.

“Nimekutana na wakulima na viongozi wa Amcos (vyama vya msingi) bado wanalalamika kasi ndogo ya malipo na waliolipwa ni wale wenye mzigo mdogo,” alisema Bungara maarufu pia kwa jina la Bwege ambaye ni mbunge wa Kilwa Kusini (CUF).

“Kwa kifupi hata hawa viongozi wa vyama vya msingi hawajui kinachoendelea kuhusu malipo haya.”

Mwenyekiti wa Amcos ya Luyaya, Ahmadi Sadi alisema kasi ya malipo ni ndogo tofauti na matarajio yao na waliolipwa ni wale wenye kilo 1,500 za korosho na kushuka chini. “Hadi sasa hatujui kinachoendelea baada ya uhakiki kufanyika. Tunaiomba Serikali ifanye haraka kwenye malipo ya wakulima,” alisema Sadi.

Mmoja wa wakulima kutoka Kata ya Limaliao wilayani Kilwa, Bakari Natunga alisema, “Wakuliwa hawana fedha na Jumatatu (kesho) shule zinafunguliwa, sijui itakuaje. Naona kila dalili ya baadhi (ya wakulima) kushindwa kupeleleka watoto wao shule.”



Chanzo: mwananchi.co.tz