Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge ataka ukaguzi wa kiuchunguzi Tanoil

Tanoil Tanoil.png Mbunge ataka ukaguzi wa kiuchunguzi Tanoil

Thu, 2 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mbunge wa Busega (CCM), Simon Lusengekile ametaka ukaguzi wa kiuchunguzi kufanyika kwa Kampuni ya Mafuta ya TANOIL ili wote waliohusika na hasara ya Sh7.8 bilioni wajulikane na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Tanoil ni kampuni Tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)

Lusengekile ameyasema hayo leo Alhamisi Novemba 2, 2023 wakati akichangia taarifa za Kamati ya Bunge za Hesabu za Serikali (PAC) na ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Taarifa hizo ni uchambuzi wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka unaoishia Juni 30, 2023.

Akichangia Lusengekile amesema hasara hiyo imetokana na uamuzi wa kupunguza bei ya mafuta uliotolewa na watendaji bila kuzingatia kanuni wala kuwashirikisha bodi, wakurugenzi na waziri husika.

“Lakini wao wanajichukulia maamuzi, hawana kibali, wanajichukulia wenyewe, kupunguza bei haiwezekani. Wanatuzunguka wanakwenda kuuza na kuchukua cha juu. Naomba Waziri wa Nishati akaanze na hili tukubaliane CAG akafanye ukaguzi wa kiuchunguzi kuona wale waliosababisha hasara ya Sh7.8 bilioni,”amesema.

Mbunge wa Viti Maalumu, Conchesta Rwamlaza amezitaka halmashauri nchini kuacha kuwa na roho mbaya na badala yake kuwalipa wazabuni wanaowadai.

“Ukitaka kufa masikini nchi hii fanya kazi na halmashauri, utatembea kudai hadi visigino vikatike na kwa taarifa za chini zinasema kama hujatoa kitu chochote hulipwi,” amesema.

Amesemawakandarasi hao wamekuwa wakisambaza hadi wanakufa bila kulipwa fedha zao jambo ambalo ni baya.

Kwa upande usimamizi, Rwamlaza amesema sektarieti za mikoa hazimii vizuri miradi iliyoko kwenye halmashauri.

“Sektarieti zitoke ziwajibike zitoke ofisini, watoke waende kuangalia hii miradi ili fedha za wananchi ziwezekutumika ipasavyo,”amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live