Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbunge aipa BoT siri ya kununua dhahabu sasa, kuiuza baadae nje

GOLD Mbunge aipa BoT siri ya kununua dhahabu sasa, kuiuza baadae nje

Sat, 25 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

KATIKA kujihami na anguko la kiuchumi kutokana na mlipuko wa virusi vya corona, Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige, ameishauri Benki Kuu Tanzania (BoT) kununua dhahabu kwa wingi, ili baadae wauze nje kwa faida.

Alisema kutokana na hali hiyo, kuna uwezekano wa uchumi wa dunia kutetereka, hivyo BoT kama watakuwa na dhahabu ya kutosha wataweza kuuza kwa bei nzuri itakayoipatia fedha za kutosha.

Alisema kutokana na ugonjwa huo, kuna mataifa makubwa uchumi wao umetetereka, hivyo kabla athari haijafika nchini, ni heri BoT wanunue dhahabu.

“Dhahabu katika soko la dunia bado iko juu, ingawa katika soko la ndani imeshuka, hivyo BoT ingeangalia uwezekano wa kununua dhahabu nyingi ili baadae waweze kuuza na kupata faida kubwa,” alisema Mbunge huyo.

Aidha, Maige alisema hivi sasa Ulaya dhahabu imepanda bei kwa kuwa wale walioweka hisa katika makampuni makubwa wanaanza kuuza kwa kuhofia anguko la kiuchumi, wanaona watapoteza fedha zao, hivyo wanaamua kununua dhahabu ili kuwekeza.

Aidha Mbunge huyo aliitaka Wizara ya Fedha kuingilia kati suala hilo, kwani lina maslahi kwa nchi, hivyo kujihami na anguko la kiuchumi kwa kununua dhahabu na kuhifadhi ni jambo jema.

Maige alisema kuwa Waziri wa Madini, Dotto Biteko, alipokuwa akiwasilisha bajeti ya Wizara yake, alisema suala la kununua dhahabu linafanywa na STAMICO, lakini hilo halizuii BoT nao kununua.

“Napenda kushauri ili suala la kununua dhahabu wasiachie sekta binafsi, BoT wanakaa na pesa nyingi, kwani badala kukaa na pesa, usikae na dhahabu ambayo ina thamani kubwa ambayo hata baadae ukiuza inakupatia fedha nyingi,” alieleza Maige.

Maige alisema endapo serikali kupitia BoT watanunua dhahabu, wachimbaji wadogo watapata fedha, lakini pia itapata faida kubwa pindi watakapoamua kuiuza.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live