Wakati Bunge likijadili ripoti za kamati za Bunge kuhusu ubadhirifu uliofanywa na baadhi ya watendaji katika miradi mikubwa. Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Judith Kapinga ameishukia Mamlaka ya Bandari (TPA) kwa kile alichokiita uozo katika ujenzi wa bandari ya Tanga.
Hoja za wabunge ziliibuliwa ikiwa ni siku ya tatu tangu Bunge lilipoanza kujadili taarifa za Kamati za Kamati ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu ripoti ya Mdhibiri na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Miongozi mwa miradi iliyotajwa kwenye kasoro ni Bandari ya Tanga, Kiwanja cha ndege cha KIA, utendaji katika halmashauri na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB).
Akichangia taarifa ya CAG iliyowasilishwa bungeni na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) jana Novemba 4, Mbunge wa viti Maalumu (CCM) Judith Kapinga alidai kuwa kuwa mkandarasi CHEC (China Harbour Engineering Company), alitafuna Sh64 bilioni ambazo alipaswa kumlipa mkandarasi mbia.
Katika mchango wake Kapinga ameitaka Serikali kumulika wahusika wote ambao wameshindwa kutimiza wajibu wao.
Kwa mujibu wa Mbunge huyo kazi hiyo aliyompa mkandarasi mbia ilipaswa kulipwa Sh104 bilioni, lakini mbia huyo aliambulia Sh40 bilioni pekee na akahoji vyombo vya ulinzi na usalama viko wapi hasa Takukuru, Katibu Mkuu wa Wizara na Waziri mhusika.
“Mkandarasi mkuu kampuni ya CHEC baada ya kusaini mkataba na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari wa Sh176 bilioni, akaenda kuigawa kazi ile kwa mkandarasi kwa gharama za chini.
“Mkataba huo unazuia kutoa kazi kwa mkandarasi mbia hadi taarifa ya siku 28, cha ajabu hii kampuni mama ilitoa tenda kwa kazi ya kuongeza kina cha maji tena siku moja kabla ya siku ya kukabidhiwa kazi hiyo ni ajabu kweli,” amesema.
Amesema kazi hiyo ilikuwa ni kuongeza kina na ujenzi wa gati na ilikuwa ikigharimu asilimia 60 ya fedha zote.
“Ile kazi ya Sh104 bilioni ndiyo akampa mkandarasi mbia, lakini badala ya kumpa Sh104 bilioni, akampa Sh40 bilioni,” amesema
Amesema mradi wa upanuzi wa bandari hiyo ulianza Agost 3, 2019 na ulitarajia kukamilika Agost, 2020 kwa gharama ya Sh176.3 bilioni kwa kazi ya kuongeza kina cha lango, tathimini ya kimazingira na vifaa vya shughuli za kibandari.
Kwa upande mwingine, Mbunge wa Tarime Vijijini Mwita Waitara (CCM) alimwomba Rais Samia Suluhu Hassan ambaye yupo nchini China kwamba akope sheria za huko ili kusudi akija Tanzania awashughulikie wote wanaotajwa.
Waitara amesema kitendo cha kuendelea kuwaona watendaji na watumishi waliotajwa kwenye ripoti hiyo wakizidi kula viyoyozi maofisini.
Naye Mwenyekiti wa Kamati ya PAC Nagenjwa Kaboyoka alisema mapendekezo mengi ambayo hutolewa na CAG huwa hayafanyiwi kazi hata kama wabunge wakipiga kelele ndani ya bunge bado ni kazi bure.