Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbivu mbichi biashara za mtandaoni kujulikana Septemba

Online Biz REPOA Mbivu mbichi biashara za mtandaoni kujulikana Septemba

Fri, 15 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati biashara za mtandaoni zikiendelea kushika kasi na kuwa chanzo cha ajira kwa vijana wengi nchini, Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa) imeanza kufanya utafiti wa huduma za mtandao kwa lengo la kuangalia sera na sheria zinavyoweza kufanya kazi katika sekta hiyo.

Utafiti huo ambao matokeo yake ya awali yatatolewa Septemba mwaka huu, unalenga katika huduma za mtandaoni, hasa biashara zinazohusisha usafirishaji wa watu (taksi, pikipiki na bajaji mtandao) pamoja na bidhaa hasa za vyakula.

Akizungumza katika uzinduzi wa mradi huo wa utafiti Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa Repoa, Profesa Donald Mmari anasema licha ya eneo hilo kuwa kimbilio la vijana wengi kama chanzo cha ajira, bado halijafanyiwa tafiti za kutosha na kutambuliwa na sera mbalimbali.

Profesa Mmari anasema utafiti huo unalenga kuangalia ni kwa jinsi gani huduma hizo zimeweza kutoa ajira stahiki kwa vijana na wakachangia kwenye pato la Taifa kutokana na kodi pale watakapokuwa kwenye mfumo rasmi.

“Tunataka kuhakikisha wanaofanya kazi kwenye sekta hii wanapata uwakilishi katika kuelekeza changamoto zao, pia tunataka kuhakikisha mazingira ya kazi ni mazuri, kwamba wanaweza kupata fursa ya kuwa kwenye mifumo ya mafao, wachangie kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii kama zilivyo ajira nyingine,” anasema Profesa Mmari.

“Kubwa zaidi tunataka kuangalia kama misingi ya haki katika mazingira ya kazi inatekelezwa katika huduma hizi za mtandao na kama haitekelezwi, kwa kuwa ni eneo jipya basi iweze kuingia katika sheria na sera ambazo zinatungwa na Serikali.”

Profesa Mmari anasema yote hayo yanafanyika kuhakikisha utoaji wa huduma kwa njia mtandao inakuwa biashara rasmi inayotambulika na kuheshimika, huku wanaofanya biashara hizo nao wanapata maslahi yanayostahili.

Mkurugenzi wa Huduma za Ajira kutoka Wizara ya Ajira, Joseph Maganga anasema utafiti huo unafanyika wakati ambao kumekuwa na ongezeko kubwa la vijana wanaojiingiza kwenye biashara na utoaji huduma za mtandaoni, licha ya ukweli kwamba tafiti za kutosha hazijafanyika eneo hilo.

Anasema kufanyika kwa utafiti huo kutaiwezesha Serikali kutambua mchango wa sekta hiyo katika pato la Taifa na utengenezaji wa ajira pia utaiwezesha kufanya maboresho ya sera na sheria kulingana na uhitaji wa biashara hizo zinazohusisha teknolojia inayobadilika kila siku.

“Natokea katika wizara ambayo inahusika na suala zima la ajira, tunahusika kwenye uandaaji wa sheria na sera mbalimbali, lakini nikiri wazi kuwa eneo hili la ajira zinazozalishwa na huduma za mtandaoni hatujalifanyia kazi vya kutosha,” anasema Maganga.

“Yako mengi hatuyafahamu, sasa inapotokea wadau wanafanya utafiti inatupa matumaini kwamba tutapata mengi kupitia utafiti huo.

“Ni ukweli usiopingika, maendeleo ya teknolojia yanafanya kazi na ajira nyingi zihamie huko kwenye mitandao, hivyo ni lazima tuwe na taarifa za kutosha ili mambo muhimu yaweze kuingizwa kwenye sera na sheria zetu. Tunasubiri matokeo ya utafiti huu ili yatusaidie sisi na wadau wetu. Masuala ya kazi yana wadau watatu ambao ni waajiri, serikali na wafanyakazi,” anasema Maganga.

Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Mtandaoni (Toda), Neema Mushi anasema wengi wanaofanya kazi hiyo wanapitia changamoto lukuki, ikiwamo ya kukosa mikataba ya uhakika na stahiki muhimu ambazo anapaswa kupata mfanyakazi.

“Tumepitishwa kwenye wasilisho la namna ambavyo watoa huduma za mtandao wanapaswa kuwa, ni wazi sisi tupo nyuma kabisa, mikataba kwetu imekuwa changamoto, hii inamfanya mtu kufanya kazi akiwa na msongo wa mawazo, hatupati malipo stahiki, mawazo yetu hayasikilizwi na ndiyo maana nasema bora utafiti huu ufanyike huenda mambo yakiwekwa wazi kuna kitu kitafanyika,” anasema Mushi.

Naye dereva wa mtandao, Matilda Mholela alisema miongoni mwa changamoto wanazopitia madereva wanawake hutokana na dhana potofu kuwa hawastahili kufanya kazi hiyo kutokana na maumbile yao.

Maeneo yanayoguswa na utafiti huu ni usafirishaji wa abiria pamoja na bidhaa kama chakula kutoka sehemu kinakoandaliwa hadi kwa mlaji, biashara ambayo inakua siku hadi siku.

Akizungumzia usalama wa biashara hiyo, Dainess Ngowi, mkazi wa Sinza anasema pamoja na kurahisisha upatikanaji wa chakula, lakini usalama wake unaweza kuwa shakani.

“Ni kweli tunakwenda na wakati unaagiza, unaletewa hadi ulipo, ila inapaswa kuwa na watu waaminifu na waadilifu,” anasema Ngowi.

“Ikitokea mtu asiye muadilifu anaweza kuchukua chakula kikiwa salama lakini akafanya vile anaweza kufanya na kumfikishia mlaji matokeo yake kikamdhuru. Hii ina maana suala la usalama wa chakula chenyewe na uadilifu wa hawa wanaosafirisha unapaswa kuzingatiwa kwa kiasi kikubwa.”

Machi mwaka huu, kuliibuka mjadala kuhusu hatua ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutaka biashara za mtandaoni kulipiwa kodi.

Mbunge wa viti maalumu, Neema Lugangira katika ukurasa wake wa Twiter, aliandika akihoji sababu ya biashara za mtandao kutotozwa kodi kuwa, “biashara ikifika mauzo ya Sh4 milioni TRA wanatoza kodi na biashara inapofikia mauzo ya Sh100 milioni wanasajili kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kutozwa kodi kulingana na faida. Kwa nini biashara za mtandao zisitozwe kodi hata zikifikia mauzo stahiki?”

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo alinukuliwa akisema biashara yoyote inayofanywa na mauzo yake kufika Sh4 milioni, mfanyabiashara anapaswa kulipa kodi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live