Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbinu 12 za kuzalisha mayai mengi kwa mfugaji-2

9372 Pic+mayai TZW

Sat, 16 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Makala haya ni mwendelezo wa makala yaliyopita juu ya mbinu 12 za kuzalisha mayai mengi kwa mfugaji. Katika makala yaliyopita, tuliona mbinu sita za mwanzo na kubakiwa na mbinu sita nyingine kukamilisha mbinu zote ambazo makala haya ya leo yataongelea.

Hivyo ni fursa nyingine kupata ujuzi zaidi katika ufugaji kwa lengo la kuboresha biashara yako ya ufugaji.

Kabla ya kuendelea na mbinu sita zilizobaki, ni vema kujikumbusha mbinu sita zilizotangulia kwenye makala yaliyopita kupata mtiririko mzuri.

Kwanza tuliona mbinu ya kwanza katika kuzalisha mayai mengi ni kuchagua mbegu bora ya kuku yenye sifa za kutaga sana.

Mbinu ya pili ilikuwa ni kudhibiti vifo vya kuku shambani. Mbinu ya tatu ilikuwa kuzingatia umri wa kuku shambani. Mfugaji asikae na kuku wazee wasiozalisha.

Mbinu ya nne ilikuwa kudhibiti uzito wa kuku wanaotaga wasinenepe sana wala kukonda sana, kwani uzalishaji wa mayai utashuka.

Mbinu ya tano ilikuwa kujenga banda rafiki kwa maisha ya kuku na mfugaji mwenyewe. Mbinu ya sita ilikuwa kuondoa kabisa kuku wasiotaga kwa sababu mbalimbali kama vile vilema, wagonjwa wasiopona, wenye maumbo madogo kuliko kawaida, majogoo wasiohitajika na mbegu ya kuku ambayo sio kusudio la mfugaji.

Mbinu hizo hapo juu zilielezwa kwa kina kama ambavyo mbinu zilizobaki zitaelezwa kwa ufasaha kwenye makala haya ya leo.

Mbinu sita mpya

Mbinu ya saba ni matumizi ya mwanga wa jua na taa za usiku. Matumizi mazuri ya mwanga yanaweza kuongeza asilimia 20 hadi 30 kwenye uzalishaji wa mayai.

Kuku ni viumbe wanaopenda mwanga sana na uzalishaji wao wa mayai hutegemea urefu wa siku. Kuku wanaokaa kwenye mwanga kwa saa 16 huzalisha mayai zaidi kuliko kuku wanaokaa kwenye mwaga chini ya muda huo.

Kadiri muda wa mwanga unavyozidi kupungua ndivyo mayai yanavyopungua. Baada ya mwanga wa jua wa saa 12, inafaa kuwasha taa kuku wapate mwanga walau saa nne za ziada. Vilevile kuku wanahitaji kupumzika, hivyo zima taa wapate giza mara baada ya saa nne hizo kupita.

Mbinu ya nane ni chakula na ulishaji. Chakula bora na ulishaji unaotakiwa ndiyo uwezo wa kuku kutaga zaidi. Lisha mara mbili, mapema asubuhi na jioni jua likiwa limepoa. Zingatia kiasi kinachotakiwa kuku kula kwa siku.

Mbinu ya tisa ni kudhibiti joto bandani. Kuna wakati joto linakuwa kubwa kiasi cha kuku kushindwa kula vizuri au kunakuwapo na baridi kupita kiasi. Mabadiliko ya joto hushusha mayai sana, hivyo mfugaji anatakiwa kujua hili.

Wakati wa joto usiweke kuku wengi sana bandani, weka madirisha mengi ya kutosha, wape maji mengi ya kunywa pia lisha mapema alfajiri na jioni sana kukiwa kumepoa.

Epuka kunywesha maji yaliyokaa kwenye jua na kuchemka kama vile maji yaliyoko kwenye tanki la juu ya paa. Maji yaliyopata moto hayafai kunywesha kuku. Unaweza kufunika au kuweka kivuli kwenye tanki ili maji yasipate joto.

Mbinu ya 10 ni usimamizi. Kagua kila mara kujua kila kitu kwenye mabanda ya kuku kuanzia hali ya kiafya kwa kuku wako, kiasi cha chakula wanachopewa, muda wanaopewa chakula, usafi wa vyombo na mazingira

Pia, takwimu za idadi ya kuku bandani na mayai wanayotaga. Mambo haya ni muhimu sana kuziba mianya inayopunguza mayai kwenye shamba lako.

Mbinu ya 11 ni kuzingatia chanjo za kuku kwa magonjwa yenye chanjo na kuweka miundombinu yenye kuzuia magonjwa kuingia shambani kwako.

Kwa kiasi kikubwa magonjwa huletwa na binadamu na wanyama au ndege wanaoingia shambani. Kuweka uzio au chochote cha kuzuia watu au wanyama na ndege kufika shambani, ni njia salama kwenye mradi wako.

Kuweka kumbukumbu ya chanjo zote muhimu ni bora kuliko kusubiri kutibu kuku wakiugua. Baadhi ya magonjwa hayatibiki, hivyo suluhisho lake ni chanjo tu.

Mbinu ya 12 ni kutengeneza viota vya kutagia vilivyo safi na kuokota mayai kila mara bandani. Wafugaji wengi hupoteza mayai mengi kwa kuchelewa kuokota mayai, matokeo yake mayai huvunjika, kuchafuliwa na mbolea ya kuku na mengine kuliwa na kuku.

Okota mayai kila mara hasa muda wa asubuhi hadi saa sita mchana, kwani kuku hutaga zaidi. Kuacha mayai yajae kwenye vitagio ni kushawishi kuku kula mayai.

Usiache kuku watage kwenye sakafu, wala usiweke vitagio vichache bandani kwa kuwa kuku watavunja sana mayai. Kuku wakizoea kula mayai ni vigumu kuwazuia hata kama utaboresha chakula chao.

Ikiwa hali hii ya kula mayai imeshamiri, angalia viota vyako huenda sio rafiki kwa utagaji wa kuku kisha rekebisha.

Chunguza lishe ya chakula chao kama ina upungufu kwa sababu upugufu wa lishe hulazimu kuku kula mayai.

Ukifanya yote hayo lakini bado kuku wakawa wanakula mayai, basi kata midomo yao iwe butu. Kuwa mwangalifu wakati wa kukata; usikate sana wakashindwa kula. Tumia kifaa maalumu cha kukata na kupunguza damu isivuje.

Chanzo: mwananchi.co.tz