Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbarawa akerwa na utendaji TRC

Mbarawa Makame Mbarawa akerwa na utendaji TRC

Wed, 11 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa ameonyesha kutoridhishwa na utendaji wa menejimenti ya Shirika la Reli Tanzania (TRC) hususani katika kusafirisha mizigo ambapo hutumia mwezi mzima kusafirisha saruji kutoka Tanga mpaka Kigoma jambo linalosababisha shirika hilo kuendeshwa kwa hasara.

Hayo yamebainika katika mkutano wake na wafanyakazi wa TRC uliofanyika katika Stesheni ya reli Kigoma baada ya kubaini kuwepo kwa kontena zilizosafirishwa kutoka mkoani Tanga kwa takribani siku 24, jambo ambalo Waziri Mbarawa amelitafsiri kuwa ni kukosa uwajibikaji kwa viongozi wanaolisimamia shirika hilo.

"Siku 24 haya mabehewa pengine yatatoka kesho au kesho kutwa mtapataje faida kila siku mtahangaika na wafanyakazi watalalamika tu, kuwa meneja maana yake ni kutafuta majibu ya changamoto," alisisitiza Prof. Mbarawa.

Awali akizungumza katika mkutano huo Kaimu Mkurugenzi Mkuu TRC, Mhandisi Senzige Kisenge amesema shirika hilo limeendelea kuimarika kimapato kutoka makusanyo ya shilingi bilioni 34 kwa mwaka 2015/16 hadi kufikia shilingi bilioni 54.7 mwaka 2022/23.

Aidha kwa upande wao baadhi ya wafanyakazi wa TRC wakizungumza mbele ya Waziri Mbarawa walibainisha changamoto mbalimbali zinazolikumba shirika la reli nchini kuwa ni pamoja na uhaba wa wafanyakazi, kutokulipwa kwa wakati kwa fedha za muda wa ziada pamoja na jengo la abiria kukosa runinga kwa ajili ya wasafiri.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live