Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mbao kuviingizia vijiji Sh bil 1.3

89feda5b62c93bdef6a2b5c4cad38b6e.jpeg Mbao kuviingizia vijiji Sh bil 1.3

Wed, 17 Mar 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

VIJIJI vinne vya Mkoa wa Ruvuma vinatarajiwa kuingiza Sh 1,349,062,373 kwa kuuza mbao za mita za ujazo 5,236.28 mwaka huu.

Vijiji hivyo vya Litowa, Liweta, Muhukuru Lilahi na Ndongosi vinatekeleza mpango wa usimamizi wa hifadhi za misitu ya vijiji katika Halmashauri ya Songea.

Vijiji hivyo vilitoa taarifa hiyo wakati wa uzinduzi wa mtambo wa kuchakata magogo wa kisasa ulionunuliwa kutoka Canada ili kuchochea juhudi za vijiji hivyo kuongeza thamani ya bidhaa za misitu na kuchangia katika uchumi wa viwanda.

Akisoma taarifa ya usimamizi shirikishi wa hifadhi ya misitu ya vijiji vya Halmashauri ya Wilaya ya Songea, mmoja wa viongozi wa vijiji, Kaspari Mhongo, alisema fedha hizo ni mtaji mkubwa katika kuhamasisha utunzaji wa misitu.

Alisema vijiji hivyo vimeandika mpango kazi kwa kushirikiana na Programu ya Mnyororo wa Thamani wa mazao ya Misitu (FORVAC), Shirika la Kuhifadhi Mpingo na Maendeleo (MCDI) na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) umeshapitishwa.

Vijiji hivyo vipo katika mpango unaohusu vijiji saba. Vijiji vingine vitatu bado vinaendelea na kutekeleza mpango kazi kuwezesha kuvuna rasilimali hizo.

Mkurugenzi wa MCDI, Jasper Makala, ambaye taasisi yake ni mwezeshaji, alisema matumizi ya mashine hiyo yatawezesha wanavijiji hao kupata faida mara mbili ya matumizi ya misumeno ya kawaida.

Pamoja na utoaji wa mitambo hiyo ya kuchakata, MCDI pia imeshatoa mtambo wa kukaushia unaotumia nguvu za jua wenye uwezo wa kukausha mita za ujazo 20 za mbao na hivyo kuongeza ubora wa mbao.

Akizindua mtambo huo juzi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro, alisema uwepo wa mtambo huo utasaidia kuhifadhi mazingira na kutoa tija katika mazao ya misitu.

Chanzo: www.habarileo.co.tz