Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maziwa ya nje sasa kodi ya ‘kufa mtu’

20573 Pic+maziwa TanzaniaWeb

Thu, 4 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Hatua ya Serikali kuongeza tozo ya kuingiza maziwa na bidhaa zake kwa zaidi ya asilimia 1,200 imeishtua sekta ya maziwa kiasi cha wadau wake kukutana jana kwa dharura.

Tozo hiyo ambayo ipo katika kanuni zilizotolewa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi, imepanda kutoka Sh150 kwa kilo moja mpaka Sh2,000 sawa na ongezeko la asilimia 1,233.

“Hizi si kanuni bali ni (marufuku ya kuingiza maziwa nchini) total ban. Haiwezekani tozo ikapanda kwa kiasi hicho. Bidhaa zetu hazitauzika tena,” alisema mkurugenzi wa kampuni ya Woodland Dairy nchini, Kariras Alando.

Kampuni hiyo yenye makao makuu yake nchini Afrika Kusini inasambaza maziwa aina ya First Choice nchini na Alando alisema biashara imekuwa ngumu na kwamba kanuni hizo zimewashtua kwa kiasi kikubwa.

Agosti 18, Waziri Luaga Mpina alisaini kanuni hizo mpya za huduma za mifugo na bidhaa zake ambazo zimeanza kutumika juzi na kuwatisha baadhi ya waingizaji wa bidhaa hizo nchini ambao walilazimika kukutana jana jioni jijini hapa.

Mmoja wa wajumbe wa mkutano huo aliiambia Mwananchi kuwa biashara yao imetikiswa na hawana uhakika wa kuendelea nayo kwa mabadiliko yaliyotangazwa.

“Tunalifahamu soko letu. Bidhaa zitakuwa na bei kubwa sana ambayo wateja hawawezi kununua. Tunaenda kukutana kushauriana tunachoweza kufanya,” alisema.

Kwa mabadiliko hayo ya kanuni za wizara, mdau huyo alisema huenda mabadiliko hayo yasisaidie kuongeza mapato ya Serikali na taasisi zake na kwamba yatapunguza hamasa ya unywaji maziwa na ulaji wa bidhaa zake pia.

Katibu mkuu wa wizara hiyo, Profesa Elisante ole Gabriel alithibitisha kupitishwa kwa kanuni hizo: “Ndio, waziri ametia sahihi kanuni mpya.”

Waagizaji

Tanzania ni nchi ya tisa duniani na ya tatu Afrika kwa wingi wa ng’ombe lakini inazalisha kiasi kidogo cha maziwa kutokana na mifugo mingi kutunzwa kienyeji hali inayochangia matumizi yake nchini kuwa chini ya viwango vya kimataifa.

Wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) likipendekeza unywaji wa walau lita 200 kwa mwaka, takwimu zinaonyesha kuwa kila Mtanzania hunywa wastani wa lita 45 tofauti na Wakenya wanaokunywa lita 145.

Kwa hatua hiyo, wateja waliokuwa wananunua kopo la lita moja kwa Sh3,200 sasa hivi bei itapanda kwa zaidi ya asilimia 75 hivyo kutakiwa kulipa takriban Sh6,000 kwa kiasi hicho hicho.

Mmoja wa wadau wa sekta ya maziwa nchini, Samuel Makubo alisema hili ni pigo si kwa waagizaji tu, bali sekta nzima ya maziwa.

“Uzalishaji nchini haukidhi mahitaji. Viwanda vya maziwa vitashindwa kuagiza malighafi na vikilazimisha, basi bidhaa zao zitauzwa kwa bei kubwa. Wananchi tutalazimika kunyang’anyana kiasi kidogo kinachozalishwa nchini,” alisema mdau huyo.

Alisema viwanda vya kusindika maziwa nchini, vinahitaji lita 700,000 lakini huzalisha asilimia 40 ya uwezo uliopo kutokana na uhaba wa malighafi.

Takwimu zinaonyesha kuwa Tanzania hutumia zaidi ya Sh165 bilioni kuagiza maziwa kutoka sehemu tofauti duniani kujaza pengo lililopo.

Meneja wa kampuni ya maziwa ya KCC nchini, Marigo Chacha alisema wasambazaji na mawakala ndio watakaoathirika zaidi kutokana na hatua hiyo kwani wamewekeza fedha nyingi na kuajiri vijana wa kuwasaidia kufanikisha biashara yao.

“Tanzania hatuzalishi siagi wala samli, tunaagiza kutoka nje. Mabadiliko haya yanaweza kusababisha mgogoro na nchi tunazofanya nazo biashara endapo zitaamua kupandisha tozo kwenye bidhaa zetu pia,” alisema Chacha.

Alando alisema kampuni yake ilikuwa inaingiza kati ya lita 450,000 na 500,000 za maziwa aina ya First Choice kila mwezi lakini imelazimika kusitisha kufanya hivyo kwanza.

“Wakati wote huwa kunakuwa na mzigo unaosafirishwa kuja nchini. Mabadiliko yaliyotangazwa yametufanya tusichukue kibali kingine chochote kuanzia Oktoba Mosi kanuni hizi zilipoanza kutumika. Tunafahamu, wateja wetu hawatamudu bei mpya,” alisema.

Wasindikaji

Maziwa si jambo la Muungano, kwa hiyo yale yanayozalishwa Zanzibar yakija Bara huhesabika yanatoka nje ya nchi hivyo kutakiwa kulipiwa tozo zote zilizopo kwa mujibu wa sheria.

Hivi karibuni, Serikali ilizishikilia zaidi ya lita 100,000 za maziwa ya kampuni ya Azam iliyo chini ya Said Salim Bakhresa (S.S.B) jambo lililoathiri usambazaji wa bidhaa hiyo. Wizara ilikuwa inaitaka kampuni hiyo kulipa tozo ya Sh150 kwa kila lita.

Hata hivyo, msemaji wa kampuni za Bakhresa (BGC), Hussein Sufian alisema: “Tulitii sheria. Tulilipa tozo husika na kuruhusiwa kuondoa maziwa yetu. Tumeshayaingiza sokoni.”

Wakati waingizaji wa maziwa wakilalamika kwa hofu ya kupoteza biashara, wasindikaji wa ndani wanashangilia kwa kupewa fursa kubwa wanayotakiwa kuichangamkia.

“Tunaipongeza Serikali kwa uamuzi huu. Itaongeza motisha kwa wafugaji na kuvutia wawekezaji zaidi. Naamini watajitokeza wazalishaji wa maziwa ya unga,” alisema Fuad Jaffer, mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Asas iliyopo mjini Iringa.

Alifafanua kuwa kuzuiwa kwa maziwa ya unga kuingia nchini, kutawapa nafasi wasindikaji wa ndani kujijenga na kuweza kushindana hata kimataifa.

Sekta hiyo inasimamiwa na Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) ambayo mkurugenzi mtendaji wake, Jeremiah Temu hakuwa na la kusema kuhusu mchango wa mabadiliko hayo kuendeleza viwanda na sekta kwa ujumla.

“TDB ni mtoto na wizara ni baba. Mzazi ndiye huamua nini kifanyike kwa wakati gani. Huo ni uamuzi wa wizara,” alisema Temu.

Chanzo: mwananchi.co.tz