Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mazingira bora uwekezaji yanavyoboresha ukusanyaji wa kodi kampuni za simu

485936a4ec05cf40d11360d954ce8766 Mazingira bora uwekezaji yanavyoboresha ukusanyaji wa kodi kampuni za simu

Mon, 24 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

KAMA umekuwa mdadisi wa sekta ya mawasiliano nchini Tanzania kwa miongo miwili ama zaidi, unaweza kukubaliana nami kuwa kumekuwepo na mijadala na maswali kadhaa juu ya ulipaji kodi wa kampuni za simu hapa Tanzania.

Mara nyingine kumekuwa na utata kuhusu kiasi cha kodi kinacholipwa na kampuni za mawasiliano zikiwamo za simu.

Mwaka 2015 Shirika la Kimataifa la Kampuni za simu za mkononi (GSMA), lilitoa ripoti maalumu iliyohusu utozaji kodi katika sekta ya mawasiliano Tanzania (“Digital inclusion and mobile sector taxation in Tanzania”).

GSMA ilikadiria kuwa kampuni za simu za mkononi zinachangia zaidi ya asilimia 11 ya makusanyo ya kodi nchini Tanzania.

Sera bora za uwekezaji na za kikodi ndizo zinazotajwa kubeba kampuni kubwa zaidi za mawasiliano za Vodacom, Airtel na Tigo na kuzifanya kuwa miongoni mwa kampuni kubwa za mawasiliano zinazoaminika kwa wananchi hapa nchini.

Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Hisham Hendi anasema sera bora za uwekezaji na za kikodi zilizowekwa na serikali zimekuwa chachu kwa mafanikio ya kampuni za simu na pia katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

“Kwa kuzingatia ukubwa wa kijiografia wa Tanzania, kwa kampuni za simu hususani anayoisimamia, wamefanya uwekezaji mkubwa wa miundombinu, lakini zaidi, sera bora za uwekezaji na za kikodi za Serikali…”

“Ni kazi ya pamoja kati ya serikali na sekta binafsi na iliyohitaji kujitolea pakubwa. Kwa mfano, Serikali haikupata kodi ya mapato kwa muda fulani kwa vile ilitoa motisha kubwa za uwekezaji.

Serikali haikupata pia ushuru wa forodha, lakini kampuni za simu ziliwekeza pakubwa. Kati ya mwaka 2012 na 2020, Vodacom pekee imewekeza zaidi ya Sh trilioni 1.6 nchini Tanzania,” anasema Mkurugenzi huyo.

UMILIKI SOKO LA MAWASILIANO

Ripoti ya karibuni ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), inaonesha kuwa, hadi mwezi Machi mwaka huu, kampuni za simu zinahudumia wateja zaidi ya milioni 48. Katika hao, Vodacom inaongoza kwa kuwa na wateja milioni 15 (sawa na asilimia 32 ya soko).

Vodacom inafuatiwa na Airtel yenye wateja milioni 13 (sawa na asilimia 27 ya soko) kisha inafuata kampuni ya Tigo yenye wateja milioni 12 sawa na asilimia 26 ya soko la huduma za simu nchini. Mazingira bora uwekezaji yanavyoboresha ukusanyaji wa kodi kampuni za simu.

FAIDA KUU ZA KUKUA HUDUMA ZA SIMU

Kwa wastani, kodi inayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ni karibia asilimia 60 ya bajeti ya Serikali. Kwa Mujibu wa TRA, Mwezi Desemba mwaka 2019, Mamlaka hiyo iliweka rekodi ya juu kabisa ya ukusanyaji mapato. Ilikusanya Sh trilioni 1.987.

Matumizi ya mashine za kielekroniki za kodi (EFD), ni mojawapo ya sababu za mafanikio hayo. Mashine na mfumo wa EFD unategemea huduma za simu, hasa data.

Pamoja na vifaa vingine, mashine ya EFD ndani yake inawekwa “laini ya simu” ili iweze kuwasiliana na mfumo uliopo TRA.

GSMA, katika ripoti yake inataja kuwa faida za huduma za simu zimewezesha TRA kufikia malengo ya makusanyo ya kodi ilitokana na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).

Faida nyingine ni ujumuishwaji wa wananchi kidigitali ambapo Watanzania, kwa mamilioni sasa wanaweza kuzifikia na pia kunufaika na huduma za simu za mkononi.

Aidha, ujumuishwaji wa wananchi kwenye mifumo ya kifedha ni faida ya nyingine inayotajwa kwa maana kuwa, watu wengi zaidi wanaweza kupata huduma za kifedha na za kibenki kupitia simu zao.

Nyingine muhimu ilikuwa ni ukuaji na utulivu wa kiuchumi unaotoa mchango wa moja kwa moja katika uzalishaji na kukuza uchumi wa Tanzania.

Kwa kuzangatia tija ya uwepo wa huduma za simu, Hendi anasema katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, Vodacom pekee imelipa serikalini kodi, ada na tozo mbalimbali zinazofikia Sh trilioni 1.9.

“Huduma zimeenda sambamba na ulipaji kodi. Kwa kampuni ya Vodacom, ulipaji wa kodi ulikuwa kwa wastani wa asilimia 8 kila mwaka.

Kutoka Sh bilioni 324 mwaka 2016 mpaka kufikia Sh bilioni 435 mwaka 2020,” anafafanua Mkurugenzi huyo.

Chanzo: habarileo.co.tz