Serikali nchini, imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa mafuta ya kula kwa kufanya mageuzi makubwa katika mazao ya mafuta, ikiwemo michikichi ambao umeingizwa katika orodha ya mazao ya kimkakati.
Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde ameandika kuwa Serikali ilichukua hatua za kuliingiza zao la michikichi katika orodha ya mazao hayo kama ilivyo kwa pamba, tumbaku, kahawa, korosho, chai, mkonge, zabibu na alizeti.
Ameendelea kuandika kuwa, “hiyo inaendelea na uzalishaji wa mbegu na miche bora ya michikichi aina ya TENERA inayotoa mafuta mara tatu zaidi ya aina ya DURA, ambayo inalimwa na wakulima kwa takribani asilimia 90.”
Mavunde ameongeza kuwa, “Hadi kufikia Januari, 2023 TARI Kwa kushirikiana na kampuni binafsi imezalisha jumla ya mbegu milioni 14.14. Kati ya hizi, mbegu milioni 11.59 zimezalishwa na TARI na mbegu milioni 2.54 zimezalishwa na kampuni binafsi zikiwemo FELISA, NDF na Yangu Macho Group Ltd.”
Aidha, Mavunde alimnukuu Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyesemavkati ya mbegu milioni 14.14 , zilizozalishwa, mbegu milioni 9.60 zimekwisha sambazwa na kuoteshwa na taasisi mbalimbali zikiwemo JKT na Magereza, Halmashauri zote nane za mkoa wa Kigoma, Halmashauri 25 za nje ya mkoa wa Kigoma, vituo vya TARI na Wakala wa Mbegu za kilimo Tanzania (ASA).
Hata hivyo, alimaliza andiko lake kwa kusema hadi kufikia Januari, 2023 jumla ya miche 3,122,566 imepatikana ambapo miche 1,968,087 imegawiwa kwa wakulima ndani na nje ya mkoa wa Kigoma na kwamba pia wataendelea kuchukua maoni ya wakulima na wadau.