WAZIRI wa Uwekezaji, Geofrey Mwambe na Waziri Biashara na Viwanda, Kitila Mkumbo leo wanakutana na Uongozi wa Kiwanda cha Kuzalisha Saruji cha Dangote mkoani Mtwara kufuatia mgomo wa madereva wa kiwanda hicho ambao umedumu kwa siku 12 bila kuwa na suluhisho.
Mawaziri hao waliwasili leo mkoani hapa mapema asubuhi na kuongozana na Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Gelasius Byakanwa kwenda kwenye kiwanda hicho cha Dangote ambapo vikao vinaendelea kwa sasa.
Vikao hivyo pia vinawahusisha mawakala wa usarifirishaji na uongozi wa madereva wa kiwanda hicho.
Hata hivyo mapema leo, Mkuu wa Mkuu wa Mkoa Byakanwa aliwaambia waandishi wa habari kuwa wanatarajia kufanya vikao vitatu vya ndani na kisha kutoa taarifa kwa umma kuhusiana na yatakayojiri kwenye vikao hivyo.
Vikao hivyo vinakuja siku chache baada ya madereva kugoma kwa kile walichodai kuwa ni : stahiki za msingi ikiwa ni pamoja na nyongeza ya mshahara, posho za safari, kulipiwa faini za barabarani.
Madai yao mengine ni mikataba ya ajira.
Awali uongozi wa kiwanda cha Dangoylte ulifanya kikao cha maridhiano na madereva hao wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Byakanwa na kukubali kulipa faini za barabarani, ufungaji wa maturubai na kuongeza gharama za kutoa gari kiwandani kwenda bandarini.
Lakini pamoja na makubaliano hayo, madereva hao wameendelea kugoma huku wakidai kuongezwa mishahara kupatiwa mikataba ya ajira na posho za safari.