Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawaziri wakutana maagizo ya Samia

4350471ded399feae2395ca12225bf9e Mawaziri wakutana maagizo ya Samia

Fri, 16 Apr 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk Faustine Ndugulile na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa wamefanya kikao na makatibu wakuu na manaibu katibu wakuu kujadili hoja zinazohusu utekelezaji wa majukumu ya sekta ya mawasiliano na utangazaji nchini.

Taarifa iliyotolewa na kitengo cha mawasiliano serikalini katika Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari jana ilieleza kuwa, kikao hicho kilichohudhuriwa na wataalamu kutoka wizara hizo, kilijadili hasa suala la televisheni za mtandaoni kwenye vipengele vya usajili, kanuni, sheria, miongozo na tozo.

Viongozi wa wizara hizo walikutana jijini Dodoma kutekelezaji maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa hivi karibuni wakati akiwaapisha makatibu wakuu, manaibu katibu wakuu na wakuu wa taasisi mbalimbali aliowateuwa.

Miongoni mwa maazimio katika kikao hicho ni kuangaliwa upya muundo wa uwajibikaji wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa wizara hizo bila kuathiri utekelezaji wa majukumu ya mamlaka hiyo katika sekta ya mawasiliano na utangazaji.

Aidha, viongozi hao wamekubaliana kuzipitia upya kanuni, sheria na miongozo kuhusu televisheni za mtandaon, pamoja na kuweka mifumo rafiki ya usajili na malipo kwa kuangalia uwezekano wa kupunguza tozo na kufanya uchambuzi yakinifu wa nani anatakiwa kulipia kuendena na matumizi husika.

Katika kikao hicho TCRA iliagizwa iongeze utoaji wa elimu kwa umma kuhusu usajili, kanuni, sheria na taratibu za televisheni za mtandaoni ili ziwe wazi kwa wananchi.

Viongozi hao pia walipitia hoja zinazotakiwa kufanyiwa mapitio na maboresho ikiwa ni pamoja na chaneli za runinga zinazotakiwa kuonekana katika visimbuzi bila malipo.

Hoja nyingine ni kanuni za maudhui na utoaji wa adhabu kwa vituo vya redio na runinga ziwekewe ukomo kwa mujibu wa kanuni na adhabu ziwe zenye lengo la kulea na si vinginevyo.

Wajumbe waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Naibu Waziri wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kundo Mathew, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Zainab Chaula na Naibu wake, Dk Jim Yonazi, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo, Pauline Gekul na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Hassan Abbasi.

Chanzo: www.habarileo.co.tz