Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mawakala wa forodha walia mabadiliko ya utaratibu

43614 Pic+forodha Mawakala wa forodha walia mabadiliko ya utaratibu

Mon, 25 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Baada ya Shirika la Wakala wa Meli Tanzania (Tasac) kutangaza utaratibu mpya wa uondoshaji wa mizigo bandarini, Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (Taffa) kimesema kimeshtushwa na hatua hiyo kwani itaingilia mikataba ya baadhi ya wanachama wake.

Akizungumza na Mwananchi jana, Makamu wa rais wa Taffa, Edward Urio alisema hatua hiyo ni simanzi kwa mawakala wa forodha nchini ambao wengi hivi sasa wamechanganyikiwa kwa kuwa inaingilia masilahi yao.

“Sijui Serikali imejipangaje maana baadhi ya mawakala wana mkataba na kampuni za madini kushughulikia mizigo yao kwa mwaka mmoja, miwili hadi mitatu sasa sijajua mikataba hiyo itavunjwa au itakuwaje, bado sijaelewa,” alisema Urio.

Alisema viongozi wa chama hicho wanatarajia kukutana leo kujadili hatua hiyo kabla ya kuitisha mkutano wa dharura wa wadau wote ili kupata maoni yao na kulipeleka jambo hilo mbele kupitia Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF). “Kuna baadhi ya shughuli kama uondoshaji wa mafuta zilikuwa zinafanywa na mawakala lakini zimeondolewa kwa mawakala, mbaya zaidi hadi vifaa vya mashine pia hatutaruhusiwa kushughulikia uingizaji au usafirishaji wake,” alisema. Baadhi ya wanachama wao waliokuwa wanajisimamia katika uondoshaji wa mafuta ni Puma, Total na Gapco.

Kilio cha Taffa kinatokana na tangazo lililotolewa mwishoni mwa wiki na Tasac na kuchapishwa kwenye vyombo vya habari likielekeza kuanzia Machi 4 shirika hilo ndilo litashughulikia masuala yote ya forodha katika uingizaji na uondoshaji wa mizigo bandarini.

Kinachoonekana kuwashtua mawakala wa forodha ni aina ya mizigo ambayo shirika hilo litashughulikia. Tasac limesema wasafirishaji wa madini, mchanga wa madini au makinikia, mashine za uchimbaji wa madini na bidhaa za mafuta, silaha na vifaa vya kijeshi, wanyama hai na mizigo yote ya Serikali itakuwa chini yao.

Kuanzia tarehe hiyo, shirika hilo limesema hakuna mwagizaji au msafirishaji atakayeruhusiwa kuwasilisha taarifa za usafirishaji mzigo wa mteja wake kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) bila kibali chake.

Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo, Hawa Chakoma alisema mawakala wa forodha walishirikishwa na walikaa nao kwa takribani wiki moja wakichukua maoni mpaka sheria hiyo inatungwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz