Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mavunde ataka mkakati uzalishaji mbegu bora

829a9169dcee217bc9b41183c0e4ecb7 Naibu Waziri Wa Kilimo, Anthony Mavunde

Sat, 5 Mar 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Naibu Waziri Wa Kilimo, Anthony Mavunde amekitaka kituo cha Utafiti wa Kilimo (TARI) Seliani, kuhakikisha kinakuja na mkakati na ubunifu katika uzalishaji wa mbegu bora.

Pia amekitaka kuongeza maeneo zaidi ya uzalishaji mbegu, ili kusaidia kukuza zao la ngano hapa nchini kwa kuongeza uzalishaji kutoka tani laki moja zinazozalishwa hivi sasa.

Mavunde ameyasema leo jijini Arusha, wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za kituo cha TARI Seliani, ambacho kina jukumu la msingi la utafiti wa mazao ya ngano, shayiri na maharage.

“Lazima tuhakikishe tunapunguza uingizwaji wa ngano nchini kwa sisi kama nchi kuzalisha ngano kwa wingi na ninyi TARI Seliani, ndio mna jukumu hili kubwa la utafiti na ugunduzi wa mbegu bora, kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji wa ngano nchini.

“Wataalamu na watafiti mliopo hapa kama kuna heshima kubwa mtaipata ni kusaidia uzalishaji wa ngano hapa nchini, kukua na kuipunguzia nchi gharama kubwa ya fedha ya kuagiza ngano nje ya nchi.

“Lazima utaalamu wenu na elimu mlizonazo zikatafsiriwe katika maendeleo ya mkulima na kilimo cha nchi hii, ” amesema.

Amewataka kuhakikisha wanatenga eneo kubwa zaidi la shamba la uzalishaji mbegu bora za ngano na kutenga bajeti ya mifumo ya umwagiliaji, badala ya kutegemea mvua ilivyo hivi sasa.

“Wizara tutakuwa tayari kutoa ushirikiano mkubwa, ili malengo haya ya kukuza sekta ya kulima kupitia zao la ngano kuona yanafanikiwa, hasa katika eneo la bajeti ya kusimamia vituo hivi vya utafiti wa kilimo,” amesema Mavunde.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa kituo cha TARI Seliani, Rose Ubwe ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuongeza bajeti ya fedha za utafiti hadi kufikia Sh. Bilioni 11.7 kwa mwaka 2021/22 na kuahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa.

Chanzo: www.habarileo.co.tz