Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mavunde aanika mikakati ya kuikwamua sekta ya madini

MAVUNDEEEEEE Mavunde aanika mikakati ya kuikwamua sekta ya madini

Mon, 9 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema taarifa za matokeo ya utafiti wa madini utakaofanyika katika maeneo mbalimbali nchini zitawezesha mageuzi katika sekta hiyo na kuleta mabadiliko kwenye eneo hilo.

Alisema madini ni mojawapo ya sekta muhimu katika kukuza uchumi Tanzania lakini bado haijatumika ipasavyo kutokana na rasimali zilizopo hivyo atashirikiana na wenzake kuwezesha sekta hiyo kusonga mbele kwa kuwa wamejiwekea maono ya 2030 madini ni maisha na utajiri.

Alisema ikifika mwaka 2030 wanataka wawe wamefanya utafiti wa kina na kuboresha kanzidata ya jiolojia na miamba ili kupata fursa zaidi ya kujua madini yaliyopo na maeneo yaliyopo ili kutoa mchango mkubwa kwa Taifa.

"Sasa hivi eneo lililofanyiwa utafiti wa kina ni asilimia 16 katika madini tuna kitu kinaitwa 'qds' ambazo zipo 322. Qds ina ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 2,916 sawa na ekari 720,252.

"Kwa hiyo uchumi wa madini unaonekana sasa unatokana na eneo dogo sana lililofanyiwa utafiti wa madini, hiyo asilimia 16 matokeo yake katika ni kwamba mwaka wa fedha uliopita sekta ya madini iliingiza fedha za kigeni ilikuwa dola Sh3.3 bilioni.

Mavunde alisema kwa upande wa mapato ya ndani kwa mwaka wa fedha uliopita ni trilioni 2 sawa na asilimia 15 ya mchango wa kila sekta katika mapato hayo huku maduhuli yakiwa Sh 678 bilioni ambapo asilimia 40 yalichangiwa na wachimbaji wadogo wasio na utalaamu, teknolojia za kisasa wala taarifa za madini yaliyopo kwa uhakika.

"Nilivyoingia wizarani nikajiuliza kama tumefanya utafiti wa asilimia 16 kwa Qds tulionayo na haya ndio manufaa tuliyopata je tukifanya mara mbili au tutakuwa mbali zaidi, ndio maana tumekuja na maono ya ikifika mwaka 2030 tuwe tumefanya utafiti kwa asilimia 50 ili kubaini viashiri vya madini na miamba," alisema Mavunde.

Kwa mujibu wa Mavunde, mara ya mwisho Tanzania kurusha ndege kwa ajili ya kufanya utafiti ilikuwa kati ya 2013/14 na 2004 katika maeneo ya Kahama, Biharamulo, Mpanda na Nachingwea na walifanikiwa kugusa eneo la kilomita za mraba 30,000.

Mavunde alisema , maeneo yaliyofanyiwa utafiti wa kina ni machache kuliko yaliyobaki, lakini sekta ya madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa.

Hata hivyo, Mavunde alisema utafiti ukiwekezwa zaidi katika taasisi ya jiolojia na utafiti wa madini mafanikio makubwa ya uchumi yatafikiwa.

"Kupitia taarifa ndio sasa tunatumia migodi iliyopo hivyo tunayo nafasi kubwa ya kuendelea kufanya vizuri ndio maana nimejipima na kuitaka kuitoa Tanzania kutoka katika asilimia 16 kwenda zaidi ya asilimia 50 ili tupate manufaa katika Taifa letu.Teknolojia inayotumika sasa hivi ni kurusha ndege, helkopta na ndege zisizo na rubani," alisema Mavunde.

Madini ni maisha

Mavunde alisema maisha ya binadamu yanabebwa na madini, huwezi kutofautisha au kutenganisha mwanadamu na madini, akisema lengo la wizara yake ni kufungamanisha madini na sekta nyinginezo.

"Tulifanikiwa kurusha ndege, tukipiga picha na kupata viashiria, ipo miamba yenye maji mengi taarifa hii tutawapa wenzetu pia wanaohusika na huduma za maji. Wizara ya maji watajua ni wapi watachimba visima virefu vya maji ili kuwapatia huduma wananchi hapo ndipo tunaposema madini ni maisha.

"Wizara ya kilimo inakuja na mkakati mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji ili kuondokana na kilimo cha kusubiri mvua, lakini kupitia taarifa zetu watajua ni wapi kuna miamba na kuchimba mabwawa ya umwagiliaji," alisema Mavunde.

Mavunde aliyeteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kushika wadhifa akichukua nafasi ya Dk Doto Biteko aliyeteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, alisema wizara yake ndio itakayotoa taarifa wapi kuna miamba yenye maji mengi ili kuwezesha wizara nyingine.

Alisema Tanzania inaagiza mbolea lakini ina madini yanayoweza kutumika kwa malighafi ya kuzalisha bidhaa hiyo nchini.

Alisema wakimaliza kufanya utafiti ni rahisi kuwavutia wawekezaji wakubwa kuja kuwekeza nchini katika mbolea.

"Manufaa yake Watanzania watapata ajira na mbolea kwa wakati, maisha yatabadilika ikiwemo ya mkulima kutokana na uwepo wa viwanda vya mbolea. Hii ndio maana ya madini ni maisha yanakwenda kugusa maisha ya Mtanzania," alisema Mavunde.

Alisema utajiri wa madini ni taarifa na kampuni zote kubwa za kuwekeza zilianza kupata taarifa zilizowasaidia kupeleka katika taasisi za fedha za kimataifa na hatimaye kupata mitaji iliyowawezesha kuwekeza.

"Ukiwa na taarifa za maeneo yako yote nchi zima huo ndio utajiri ambao Tanzania tumeishikilia .Kama Geita Gold Mine (GGM) na Barick katika eneo dogo walilofanyia utafiti ndio wamepata mtaji mkubwa, Tanzania itakuwa katika nafasi gani endapo itakuwa na taarifa? alihoji.

Kupitia utafiti huo utaliwezesha Shirika la Taifa la Madini (Stamico), kuwa shirika linalomilikiwa na Serikali linaloongoza Afrika kwa madini likishinda na kampuni kubwa katika uwekezaji wa sekta hiyo.

"Bado tunahitaji kampuni kuja kuwekeza lakini tunataka kazi hii ifanywe na Stamico kwa kiwango kikubwa kwa sababu atakuwa na taarifa za utafiti zinaonyesha madini yako wapi ili kumpeleka mchimbaji mdogo na mkubwa.

"Leo mnashuhudia migogoro ya wachimbaji wakubwa na wadogo sababu yake ni ndogo sana wanachimba kwa kuotea mwisho wa siku wanapoteza mitaji yao.Siku zote mchimbaji mdogo akiona kuna mchimbaji mkubwa anasogea karibu kwa sababu kuna utafiti umefanyika," alisema.

Alisema kupitia utafiti utakaofanyika utawezesha mchimbaji mdogo kubaki katika eneo lake na itapunguza migogoro kati ya wachimbaji wadogo na wakubwa kwa sababu kila mtu atabaki katika eneo lake sahihi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live