Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mavunde: Utafiti utakuza sekta ya madini

MAVUNDEEEEEE Mavunde: Utafiti utakuza sekta ya madini

Sun, 22 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Dar es Salaam. Waziri wa Madini, Antony Mavunde amesema ili sekta ya madini itoe mchango katika uchumi wa nchi ni lazima utafiti wa kina ufanyike kwa ajili ya kuboresha kanzidata ya miamba kupata taarifa sahihi za madini.

“Kwa kufanya Jiofizikia "Geophysics" (ni fani ya sayansi ya miamba na dutu) kutambua madini tuliyonayo na uwezo wetu wa kuweza kuyachimba huo ndio uchawi wa kuikuza sekta yetu ya madini,” amesema.

Kauli hiyo ameitoa Dodoma leo, Oktoba 21 kwenye uzinduzi wa mitambo ya kuchorongea madini kwa wachimbaji wadogo na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) hafla iliyohudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema nchi ya Tanzania imegawanywa kwenye vipande 322, kila moja inaurefu wa kilomita 54 sawa na upana wake ni kilomita hizo 54.

“Kwa pamoja zinatengeneza eneo la kilomita za mramba 2,916 sawa na ekari 72,252, utafiti ulifanyika nchini bado hauwezi kutoa taarifa sahihi kwa kile kilichopo chini ya ardhi na duniani kote wanaenda kwenye teknolojia ya uchunguzi wa hali ya juu wa kijiofizikia wa anga (high resolution airborne geophysical survey),” amesema.

Amesema utafiti huo unatoa taarifa sahihi kwa kubaini madini yaliyopo kwenye miamba na kurahisisha uchumbaji wa madini.

Amesema mwaka wa fedha uliopita Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), walikusanya kodi ya mapato ya ndani Sh2 trilioni na asilimia 15 ilitoka kwenye sekta hiyo.

“Maduhuli yaliyokusanywa na serikali katika eneo la asilimia 16 ya madini ni Sh678 bilioni na kama mchango huo umepatikana katika eneo dogo la asilimia 16 tukifanya mara mbili mchango wake utakuwa mkubwa,” amesema.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa (Stamico), Dk Venance Mwasse alisema mageuzi yaliyofanywa na shirika hilo ni matokeo mazuri ya kupata vifaa hivyo vya kisasa vinavyeenda kuleta tija na kipato kwa wachimbaji wadogo nchini.

“Vifaa vilivyozinduliwa vinathamani ya Sh 9.2 bilioni lakini uwekezaji tuliofanya mwaka huu ni Sh17.3 bilioni na vifaa vingine viko kazini vikiendelea kufanya kazi,” amesema.

Amesema pamoja na kutekeleza majukumu ya kimkakati shirika hilo bado linaendelea kuwarasimisha wachimbaji wazawa kwa mafanikio na maslahi mapana kwa Taifa.

“Mitambo hii ni suluhisho kwao katika kurahisisha kazi lakini itakuwa chachu kwao kukopesheka na taasisi za kifedha tumezindua mitambo mitano kati ya 15 itakayonunuliwa na shirika inaenda kuinua kipato cha wachimbaji,” amesema

Awali, Mwenyekiti wa Umoja wa Benki Tanzania (TBA), Theobald Sabi alisema wameanza kufanya majadiliano ya vikao na viongozi wa vyama vya wachimbaji kuangalia namna ya kutoa mikopo kwenye sekta hiyo ya wachimbaji wadogo katika kuinua mitaji yao.

“Katika kikao cha kwanza kilihudhuriwa na mabenki mengi nchini, na Waziri wa sekta na matarajio yetu yaliyoazmiwa yatafikiwa na kuanza kutoa mikopo,ili kukidhi mahitaji,” amesema.

Sabi ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Biashara ya Taifa (NBC) amesema jumuiya hiyo bado inaendela kufanya tafiti za kisayansi kubaini ujazo na aina ya madini yaliyopo sehemu mbalimbali nchini.

“Kutokuwepo kwa tafiti na takwimu hizo ni kikwazo katika upatikanaji wa mikopo kwahiyo tunaamini kupitia tafiti tunazofanya huko tutakokwenda mikopo itakuwa rahisi kupatikana kwa wachimbaji wadogo,” amesema.

Pia ameipongeza serikali kwa kuja na sera ya ndani inayotoa nafasi kwa benki za ndani kutoa mchango wake na inachangia ukuaji wa kiwango cha mikopo hadi kufikia sh761.6 zilizotolewa katika sekta hiyo.

Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimba Madini Tanzania (Femata), John Bina, licha ya kuwa na kuwa na wachimbaji milioni sita nchini bado wamekuwa na changamoto ya upatikanaji wa mikopo.

“Changamoto zingine umeme, msamaha wa kodi kwenye vifaa tunavyotumia kuchimba, kutokusamehewa madeni,na mipaka yetu imekuwa shida,” amesema

Kuhusu kukabiliana na mikopo wamejipanga kuanzisha benki ya femata na kuanza mchakato wa kuwapa wachimbaji wote vitambulisho nchi nzima.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live